DRC yaifungia Al Jazeera kurusha matangazo nchini humo

Dar es Salaam. Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) imekifungia kituo cha televisheni cha Al Jazeera kutokana kile ilichokisema imerusha mahojiano na kiongozi wa kundi la waasi wa M23, Bertrand Bisimwa.

Taarifa iliyochapishwa na shirika la habari la DW, ikimnukuu msemaji wa serikali ya DRC, Patrick Muyaya akieleza kwamba mamlaka zimebatilisha kibali cha kurusha matangazo cha televisheni hiyo.

Al Jazeera yenye makao yake makuu nchini Qatar, imerusha mahojiano na Bisimwa wakati ambao kundi lake la waasi limechukua udhibiti kwenye baadhi ya eneo la mashariki mwa nchi hiyo hivi karibuni.

Muyaya amesema Al Jazeera ilirusha mahojiano hayo bila kupata kibali maalumu.

Jumatano, Al Jazeera ilirusha mahojiano ya Bisimwa, ambapo aliishutumu Serikali ya DRC kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano ya Agosti.

Baada ya kurusha mahojiano hayo, jana, Alhamisi uamuzi wa kukifungua kituo hicho ukatangazwa.

Kwa upande wake, Waziri wa Sheria wa Congo, Constant Mutamba amesema waandishi wa habari au mtu yeyote atakayeripoti kuhusu shughuli za jeshi la Rwanda na waasi wa M23, atashtakiwa.

Mashariki mwa DRC kumekuwa na mwendelezo wa mapigano kati ya Serikali na waasi hao kwa muda mrefu sasa ambapo nchi ya Rwanda umekuwa ikinyooshewa kidole kuwaunga mkono.

Hata hivyo, Rais wa Rwanda, Paul Kagame, mara kwa mara amekanusha madai ya nchi yake kuwaunga mkono waasi wa M23 wanaopigana na jeshi la DRC katika mkoa wa Kivu Kaskazini.

Taarifa iliyochapishwa na RFI imemnukuu Kagame, akizungumza na wanahabari jijini Kigali, akisema waasi hao wanaopigana, hawakutokea kwenye nchi yake.

Kulingana na Umoja wa Mataifa, mashambulizi mapya yaliyoanzishwa na M23 katika eneo la Masisi huko Kivu Kaskazini yamesababisha zaidi ya watu 100,000 waliokimbia makazi yao katika siku za kwanza za mwaka 2025.

Related Posts