BAO la Ali Khatib ‘Inzaghi’ limetosha kuipeleka Zanzibar Heroes fainali ya Kombea Mapinduzi 2025 baada ya timu hiyo kuibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya Kenya.
Mchezo huo uliochezwa leo Januari 10, 2025 kwenye Uwanja wa Gombani Kisiwani Pemba, Inzaghi alifunga bao hilo dakika ya 90+4 kwa kichwa akiunganisha kona iliyopigwa na nahodha, Feisal Salum ‘Fei Toto’.
Kenya ambayo ilikuwa ikisaka sare tu ili kufikisha pointi tano zitakazowapeleka fainali ya michuano hiyo, zilipofika dakika tisini na kuongezwa 15, ilionekana wachezaji wa timu hiyo wakitumia mbinu ya kupoteza muda.
Hata hivyo, mbinu hiyo ilishindwa kufanya kazi kwani baada ya kuruhusu nyavu zao kutikiswa, wakaanza kuchangamka kusaka bao la kusawazisha lakini hawakufanikiwa hadi mwisho wa mchezo wakapokea kichapo cha 1-0 na kuwafanya kumaliza na pointi nne wakati Zanzibar Heroes ikifikisha pointi sita.
Mchezo huo ulishuhudiwa kadi mbili nyekundu, ya kwanza alionyeshwa nahodha wa Kenya, Abdu Omar dakika ya 68 ambapo ilichukua takribani dakika tano kutoka uwanjani kwani awali hakukubaliana na adhabu hiyo hali iliyomfanya kugoma hadi pale alipozungumza kwa kina na Fei Toto sambamba na wachezaji wenzake kumsihi aende nje.
Dakika ya 90+9, beki wa Zanzibar Heroes, Ibrahim Ame naye alionyeshwa kadi nyekundu.
Ushindi huo unaifanya Zanzibar Heroes kuifuata Burkina Faso katika mchezo wa fainali utakaochezwa Januari 13, 2025 Uwanja wa Gombani.
Burkina Faso ilikuwa ya kwanza kufuzu fainali baada ya jana Januari 9, 2025 kuichapa Kilimanjaro Stars mabao 2-0 na kufikisha pointi saba wakati Kilimanjaro Stars ikimaliza ya mwisho kati ya timu nne shiriki ikiwa haina pointi wala bao huku timu zote zikishuka dimbani mara tatu.
Bingwa wa michuano hiyo ambayo kwa mwaka huu imeshirikisha timu nne za taifa, atakabidhiwa kitita cha shilingi milioni 100.