KIKOSI cha Yanga tayari kimeshatua Mauritania tayari kwa ajili ya pambano la raundi ya tano la Ligi ya Mabingwa Afrika kwa Kundi A dhidi ya Al Hilal ya Sudan, huku mmoja wa nyota wa timu hiyo akitoa msimamo dhidi ya wenyeji wao.
Yanga inatarajiwa kushuka kwenye Uwanja wa Cheikha Ould Boidiya, jijini Nouakchott, Mauritiana kuwakabili vinara wa kundi hili ikihitaji ushindi ili kujiweka pazuri katika kusaka tiketi ya kucheza robo fainali kwa msimu wa pili mfululizo.
Katika kuonyesha Yanga mechi wanaitaka, nahodha msaidizi wa Yanga, Dickson Job amewatoa hofu mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo kwa kuwaambia licha ya kuwa na kibarua ili kutinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini mastaa wa timu hiyo wamejipanga kuona hilo linatimia kwa lengo la kuandika historia ya kucheza msimu wa pili mfululizo.
Yanga ipo ugenini wikiendi hii kuvaana na Al Hilal ya Sudan mechi itakayochezwa Mauritania na wawakilishi hao wa Tanzania wakihitaji ushindi wa aina yoyote ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kuungana na timu hiyo ya Sudan kutinga hatua hiyo kwa mara ya pili mfululizo baada ya msimu uliopita kuicheza na kutolewa kwa penalti.
Yanga ina pointi nne ikishika nafasi ya tatu, nyuma ya MC Alger ya Algeria itakayofunga nayo pazi la Kundi A Januari 18, huku Al Hilal tayari imekusanya pointi 10 na kutinga robo fainali mapema baada ya mechi nne kwa kila timu.
Licha ya mechi hiyo kuonekana kuwa ngumu na kuiweka katika hatihati Yanga kutinga hatua hiyo kama itatoka sare au kupoteza Jumapili, huku Mc Alger ikashinda leo Ijumaa dhidi ya TP Mazembe inayoburuza mkia, Job alisema wameenda Mauritania wakiwa na lengo moja tu la kuona wanashinda ili watinge robo fainali nyingine.
Akizungumza na Mwanaspoti, Job alisema kama wachezaji wapo tayari kwa ajili ya kuipambania bendera ya Tanzania na timu kwa ujumla kuhakikisha wanavuna pointi zote tatu dhidi ya Al Hilal, licha ya kukiri wanaenda kucheza na timu bora na ambayo imekuwa ikiwasumbua mara kadhaa walizokutana katika michuano ya CAF.
“Ushindi tulioupata dhidi ya Mazembe umeturudisha katika ushindani na tuna ari kubwa, tunaenda kuikabili Al Hilal kwa kuiheshimu na tunajua tunaenda kukutana na timu bora,” alisema Job na kuongeza;
“Tunaihitaji sana nafasi ya kucheza robo fainali msimu huu, licha ya ukweli tulianza msimu kwa kusuasua hasa mechi mbili za awali tulizopoteza, kwa sasa kwa mechi hizi mbili zilizosalia kwenu ni kama fainali, ni za kufa au kupona kwa lengo la kuhakikisha tunakusanya pointi sita.”
Job aliongeza, wanajua hawezi kupata mteremko katika mechi hizo, lakini anaamini juhudi na kujitoa kwao kwa dakika zote 180 za mechi hizo ndio kitakachowapeleka hatua inayofuata.
Beki huyo wa kati, alisema benchi la ufundi, uongozi na wachezaji kwa ujumla wapo tayari kuipambania Yanga ili iweze kufikia malengo ya kucheza robo fainali kwa mara ya pili mfululizo kwenye michuano hiyo.
‘’Hii ni hatua ngumu na inahitaji ushindi ili kusonga mbele tumeondoka nchini tukiwa na nia moja tu kuja Mauritania kupambania pointi tatu muhimu, tumeanza na ushindi nyumbani baada ya kupoteza mchezo wa kwanza nyumbani,” alisema Job na kuongeza;
“Kama Al Hilal walitufunga nyumbani hata sisi tunaweza kuwafunga wakiwa kwao, naamini zitakuwa dakika 90 za nzuri za mbinu bora za makocha ndio zitakazoamua matokeo kwa upande wetu sisi wachezaji tupo tayari.”
Kuhusu mchezo wa mwisho utakaopigwa Kwa Mkapa, Job alisema hata huo wameutolewa macho zaidi na wataongeza morali zaidi ya kupambana na kuamini wanaweza kushinda na kusonga hatua inayofuata.
Yanga na MC Alger, iliyopo nafasi ya pili katika kundi hilo zitarudiana Jan 18 ambapo ushindi utaipeleka Yanga robo ikiifunga Al Hilal Jumapili hii.