Kelele na madhara yake kiafya  

Kelele zinaweza kuleta madhara ya kiafya au kuchokoza tatizo la kiafya la mgonjwa, ikiwamo wagonjwa wa shinikizo la juu la damu.

Katika maisha ya kila siku ya wanadamu tunakumbana na kila aina ya kelele, ikiwamo honi za magari, ving’ora, milio ya mipasuko kama baruti na bunduki, mingurumo ya magari na mashine za viwandani.

Vile vile katika maeneo ya mijini kumekuwepo na udhibiti holela wa kelele zinazotoka katika kumbi za burudani au klabu za usiku ambazo zimeanzishwa katikati ya makazi ya watu.

Vyanzo hivyo vya kelele vinaweza kuwa juu zaidi na kusababisha madhara ya kiafya.

Sauti hizi zinaweza kuwa katika hatua ya kuvumilika, lakini zinaweza kuzidi kupita kiwango cha ustahimilivu wa masikio na hivyo kumsababishia mtu madhara au athari mbalimbali za kiafya.

Madhara na athari zinaweza moja kwa moja kuwa katika sikio na kusababisha usikivu hafifu au kutosikia kabisa pamoja na madhara mengine, ikiwamo kichwa kuuma, kukosa utulivu wa kiakili, kusikia mlio au kelele ukiwa katika eneo tulivu, uchovu na kukosa usingizi.

Maeneo ambayo kwa kiasi kikubwa yanaongoza kuzagaa kwa kila aina ya kelele ni mijini kwenye msongamano mkubwa wa watu, magari na majengo, maeneo yenye shughuli za viwandani na madini.

Mtu mmoja anaweza kukutana na kila aina za kelele ambazo masikio huzimudu na nyingine ikashindwa kuzimudu hatimaye kuleta kero, kama si madhara kabisa.

Kimataifa kiwango cha kelele ambacho wataalamu wa afya ya masikio, koo na pua wanakiunga mkono kuwa salama kwa viwandani ni saa 8 za 90 Desibeli.

Wafanyakazi ambao duniani wanaongoza kwa kupata madhara ya sikio kutokana na aina ya kazi ni pamoja na wale wanaofanya kazi viwandani na wanajeshi.

Kutokana na kuwepo katika maeneo ambayo yana tatizo la kuzagaa kelele kiholela uwezo wa kusikia, unaweza kuwa na tatizo la muda au la kudumu.

Mfano unaweza kusikia mpasuko wa sauti kama ya baruti au tairi ukashindwa kusikia kwa muda wa dakika kadhaa, lakini baadaye hurudi katika hali ya kawaida.

Au unaweza kutosikia sauti ya mlipuko mkubwa kama vile wa mabomu na ukapoteza usikivu au ukapata usikivu hafifu wa kudumu.

Hii ni kutokana na milio hiyo kujeruhi ngoma ya sikio baada ya kupokea mzigo mkubwa wa mawimbi ya sauti yanayozidi kile kiwango cha uvumilivu cha sikio.

Eneo la ndani ya sikio ambalo hujeruhiwa kutokana na shinikizo kubwa la mawimbi na kusababisha udhaifu mkubwa wa kusikia linajulikana kama Corti.

Mawimbi yanayozidi kiwango cha uvumilivu wa eneo la ndani ya sikio yanaweza kumpata mtu mara kwa mara kiasi cha kuharibu eneo la ndani ya sikio kadiri siku unavyokutana na kelele hizo.

Seli zenye vinyweleo ndani ya sikio ambazo ni muhimu katika kusaidia kusikia huweza kupotea kidogo kidogo na huku uharibifu ukitokea pia eneo lingine la ndani ya sikio lijulikanalo kitabibu kama koklea.

Eneo hili linaweza kuharibiwa kutegemeana na aina ya mawimbi, uzito wa sauti na kipindi cha kuwepo katika eneo hilo lenye kelele.

Hivyo kwa wale ambao wako katika maeneo yenye kelele na ni vigumu kutokuwepo maeneo haya watumie vifaa tiba vyenye kupunguza ukali wa mawimbi ya sauti. Muhimu kuepuka kutumia zile spika ndogo za masikoni kila mara huku ukiwa unaweka sauti kubwa, kwani ni kama vile kuongeza ukubwa wa tatizo.     

                                                                                                               

Related Posts