Mabao yairejesha Kagera Sugar kambini haraka

BENCHI la ufundi la Kagera Sugar limepanga kuanza mapema maandalizi ya duru la pili la Ligi Kuu Bara wiki ijayo baada ya kuwapa mapumziko ya wiki tatu wachezaji, huku ikielezwa tatizo la ufungaji mabao ndilo lilicholisukuma benchi hilo kuiwahisha timu kambini.

Kagera inayoshika nafasi ya 15 katika msimamo wa Ligi Kuu yenye timu 16, ikiwa na pointi 11 ikifunga mabao 10 na kufungwa 19, ilishuka uwanjani mara ya mwisho Desemba 21, 2024 kumalizia mechi za duru la kwanza dhidi ya Simba na kupoteza kwa mabao 5-2 kwenye Uwanja wa Kaitaba, mjini Bukoba kabla ya kuwapa likizo ya wiki tatu wachezaji hao.

Meneja wa Kagera, Bernard Sikira aliliambia Mwanaspoti kuwa, baada ya kipigo dhidi ya Simba benchi la ufundi lilifanya tathmini kubwa na kubaini changamoto inayoisumbua timu hiyo ni upachikaji wa mabao, hivyo limeamua kuanza maandalizi mapema na kusajili wachezaji.

“Tunacheza vizuri, tunajilinda na kutengeneza nafasi lakini hatuna uwezo thabiti wa kutumia zile nafasi, pia tulipo siyo nafasi tunayostahili kuwepo. Hiyo ndiyo changamoto ambayo benchi la ufundi tumeifanyia kazi na tumechagua kurudi mapema kambini kuweka vitu sawa,” alisema Sikira.

Sikira mwenye Leseni D ya Ukocha kutoka Shirikisho la Soka Afrika (CAF), aliongeza; “Hilo ndilo tunalifanyia mpango mkakati tunatengeneza mbinu zetu tukirudi mazoezini, mbali ya kutengeneza timu pia tutaongeza mbinu mbadala kwa vijana ili wafunge mabao.”

Alisema ili kutibu tatizo hilo wamefanya usajili wa Moubarack Hamza kutoka Namungo na Omar Buzungu (Mtibwa Sugar) huku wakiupa uongozi mapendekezo ya wachezaji wengine watatu ili kuipa makali safu yao ya ushambuliaji katika duru la pili.

“Usajili mwingine unaendelea nadhani wiki ijayo tutaanza kuwatambulisha. Ni kweli tumefanya usajili na kila kitu kitakaa sawa kwahiyo kwenye upungufu kote tumezingatia namna ya kuongeza nguvu ili tutoke hapa tulipo twende juu,” alisema meneja huyo.

Related Posts