Kisarawe. Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe, Petro Magoti, amepiga marufuku kwa mtu au kampuni yoyote kuuza au kununua ardhi kitongoji cha Homboza Kata ya Msimbu wilayani humo, mpaka hapo atakapomaliza kushughulika na matapeli wa ardhi
Magoti amepiga marufuku hiyo leo Januari 10,2024 katika mkutano wa hadhara na wananchi uliofanyika ofisi za Kata Homboza, uliolenga kusikiliza na kutatua migogoro ya ardhi iliyokithiri katika kata hiyo.
Amesema katika kutafuta wahusika wanaosababisha hayo wamebaini kuwepo kwa madalali wa utapeli wa ardhi 28 na mpaka sasa wameshawakamata saba.
“Kutokana na hili nimeamua kusimamisha uuzaji wa ardhi Homboza, mpaka tumalizane na hawa madalali matapeli ambao wamewagharimu watu kwa kuwapiga fedha isivyo halali.
“Niwahakikishie madalali wote wa ardhi tutawakomba hadi waishe tukitoka katika ngazi ya kata, tunaenda mtaa kwa mtaa,”amesema Magoti.
Amesema kwa waliowakamata tayari wanasheria wamechakata mambo vizuri na Jumatatu huenda wakafikishwa mahakamani.
Pamoja na changamoto hizo, amewataka wananchi kufuata taratibu katika kununua ardhi ikiwemo kupita Serikali ya Kijiji au Mtaa.
Awali wananchi wa kata hiyo waliwasilisha malalamiko yao akiwamo Anua Ramadhani, mkazi wa Manzese, amedai aliuziwa kiwanja maeneo hayo na Aziza Kondo, Agosti mwaka 2024 kwa Sh1.4 milioni.
Hata hivyo amedai kuwa wakati anataka kuweka alama akakuta zimeng’olewa na kuelezwa ni cha mtu anaitwa Hashim.
“Nilipomlalamikia dalali aliyeniuzia eneo hilo akanipa hati na nilipokwenda nayo serikali za kitaa wakasema ni ya kughushi.”
Naye Raymond Rubaga, amedai aliuziwa viwanja vitatu tofauti kimoja alikinunua kwa Mwarami Ally Mkali, kwa mjumbe wa shina Rashidi Mahanyu na ikaja kugundulika kuwa eneo la Serikali.
“Nashukuru nilitoa taarifa na kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wahalifu hao walikamatwa na sasa wapo mahabusu.
Magoti amesema hawatawaonea haya viongozi watakayobainika kujihusisha na utapeli huo wakiwemo wa chama, huku akitaka waliotajwa na wananchi wafikishwe kamati za maadili za kata kujibu shutuma hizo.
“Pia wote waliokamatwa katika migogoro hii wakithibitika tutahakikisha watalipa hela kwanza walizotapeli watu ndio waende kutumikia kifungo,”amesema Magoti.