IMEELEZWA endapo makubaliano ya kimaslahi yakienda sawa baina ya timu ya Mashujaa FC na AS Vita ya DR Congo basi dili la mshambuliaji Ismail Mgunda linaweza likatiki.
Ipo hivi: Awali, Mwanaspoti liliripoti kuhusiana na Mgunda kufanya mazungumzo na AS Vita na baadaye akaonekana katika picha ya pamoja ya wachezaji wa timu hiyo, jambo ambalo uongozi ukakanusha na kusema bado ni mchezaji wao ana mwaka mmoja na nusu.
Taarifa za ndani zinasema yalikuwapo mazungumzo baina ya timu hizo, ila mambo ya maslahi ndio sababu ya dili hilo kushindwa kutiki kwa haraka.
“Ishu ni maslahi kwa sababu mchezaji huyo bado ana mkataba wa mwaka mmoja na nusu, hata mkimuuliza atasema, hivyo lazima timu ipate maslahi kwa kuuzwa kwake, ikishindikana basi tutakuwa hatuna namna nyingine atarejea tutaendelea kumpa ushirikiano wa kazi kama kawaida, maana wakati anaondoka hakutoroka aliaga kabisa,” kilisema chanzo hicho.
Alipotafutwa Mgunda kulifafanua hilo alijibu: “Narejea katika timu ya Mashujaa maana ni mchezaji wao nina mkataba wa mwaka mmoja na nusu, hivyo siwezi kuzungumza zaidi ya hilo.”
Kocha wa timu hiyo, Mohamed Abdallah ‘Baresi’ alisema Mgunda bado ni mchezaji wa Mashujaa kama mambo hayajaenda sawa atahakikisha anamjenga ili asitoke katika kiwango, kwani ni mchezaji mzuri na muhimu kwa timu.
“Kama kocha siwezi kumzuia mchezaji endapo ikitokea fursa kama hiyo namuacha aende akajitangaze na kutangaza nchi kwa sharti la kuzingatia matakwa ya viongozi wa klabu ambayo imemuajiri.
Aliongeza: “Ikishindikana sina budi akirejea tutakaa naye kumjenga kwa ajili ya maisha yake, huo siyo mwisho naamini akiendelea kujituma ataonekana tu kama alivyoonekana na timu hiyo.”