Mbowe: Hiki ni kipindi cha kupima viongozi

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe amesema shinikizo na msongo kinachopitia chama hicho wakati huu, ndicho kipimo sahihi cha uvumilivu, ustahimilivu, haiba na uwezo wa viongozi kutunza siri na kuilinda taasisi.

Amesema amewaachia wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi kuamua nani atakayekiongoza chama hicho kwa nafasi ya uenyekiti katika miaka mitano ijayo.

Mbowe ametoa kauli hiyo zikiwa zimesalia siku 11 kufanyika uchaguzi wa nafasi ya uenyekiti, ambao anagombea kutetea kiti hicho, pamoja na washindani wake Makamu wake (Bara), Tundu Lissu, Romanus Mapunda na Charles Odero.

Mbowe amesema hayo leo Ijumaa, Januari 10, 2025 alipohojiwa katika kipindi cha Power Breakfast kinachorushwa na kituo cha televisheni cha Clouds.

Ameeleza kushangazwa na wanaoshinikiza aache kugombea nafasi hiyo, akisema nyuma yao kuna makundi ya wasio wanachama na wengine walishakikimbia chama hicho.

Pamoja na mashinikizo yote, amesema wajumbe wa mkutano mkuu wa uchaguzi ndiyo wenye uamuzi wa nani anayepaswa kuwa mwenyekiti wa chama hicho kwa siku zijazo, hivyo amewaachia wao kazi hiyo.

Mbowe amesema amekuwa akiangalia wanaochochea yeye aache kugombea, kwa upande wa pili wengi hawaitakii mema Chadema na kwamba, huo si utamaduni wa chama hicho.

“Huo siyo utamaduni wetu na utamaduni huo hauwezi ukaiacha taasisi yetu salama, kwamba kiongozi unataka uongoze kwa kuwakanyaga wenzio halafu unajinasibu kwamba unafaa kuwa kiongozi wa taasisi,” amesema.

Amesema kipindi ambacho Chadema inakipitia sasa, ndicho kinachoonyesha uhalisia wa tabia, haiba na uvumilivu wa viongozi wake.

“Watoto wa mjini wanasema acha inyeshe tujue panapovuja. Kipindi cha shinikizo na msongo kama hiki ndiyo unaweza ukapima uvumilivu, ustahimilivu wa viongozi, haiba ya viongozi, uwezo wa kutunza siri za taasisi, uwezo wa kuilinda taasisi.

“Huwezi ukaibagaza taasisi unayotaka ukaiongoze kwamba imejaa rushwa halafu ukiambiwa baba basi toa mfano mmoja wa rushwa na wewe ni mwenyekiti wa Kamati ya Maadili ya chama kuhusu hiyo rushwa hebu ielezee leo tuione. Unatoka tu Mama Abdul… Mama Abdul na Abdul fedha Abdul ni mambo ya kihuni,” amesema.

Amesisitiza wana-Chadema ndiyo watakaoamua kwa kuangalia vigezo vyote hivyo, kwamba nani atakayekiongoza chama hicho na kikabaki salama.

Mbowe amesema amejenga watu wengi kwenye siasa na amekuza vipaji kiasi kwamba, hakuna kiongozi hata mmoja ndani ya Chadema anayeweza kusema hakupita mikononi mwake.

Amesema kuna wakati katika historia ya kukijenga chama hicho wamekuwa wakivuta wanasiasa maarufu wote na wabobezi kutoka maeneo mbalimbali.

“Unaweza ukawapima viongozi kwa utulivu, busara, matendo na kauli zao kama ambao wanajiona wana busara kuiongoza taasisi hii ambao wanafikiri wana haki ya kuachiwa taasisi hii, jambo jema, tuna njia nyingi za kuwapima, tunafahamiana kwa muda, kwa wakati.

“Muda unatatua matatizo mengi sana, naweza nikakaa na mtu kwa miaka 10 nisimjue ukafika wakati nikamjua nikajiuliza huyu ndiye yeye, ambaye tumeishi naye miaka 10 tumekula naye, tumelala nyumba moja tumeumia pamoja, yeye kawaje,” amesema.

Related Posts