Mmoja mbaroni, moto ukiteketeza nyumba 10,000

Marekani. Idara ya Polisi ya Los Angeles (LAPD) imesema inamshikilia mtu mmoja anayedaiwa kusababisha moto mkali uliochoma nyumba zaidi ya 10,000 na kuua watu 10 nchini humo.

Moto huo ulioanza usiku wa kuamkia Januari 9, 2025 umeteketeza nyumba za kifahari za mbele ya bahari.

Ofisa mkuu wa LAPD, Charles Dinsel ameuambia mtandao wa NewsNation jana Januari 9, kwamba mshukiwa mmoja yuko chini ya ulinzi, akihisiwa kusababisha moto huo kwa makusudi.

“Baada ya dakika 20 hadi 30, mshukiwa alikamatwa katika eneo la Woodland Hills na wananchi. Hili linachunguzwa kama uhalifu,” amesema Dinsel.

Ofisa huyo alipotakiwa kueleza moja kwa moja kama moto huo uliwashwa kwa makusudi alijibu, “kwa sasa, tunaamini hivyo.

Vyanzo viliiambia DailyMail.com kwamba mkazi mmoja aliita 911 kuripoti mtu aliyekuwa akijaribu kuwasha moto katika 21700 block ya Barabara ya Ybarra mnamo saa 10:30 alasiri.

“Tunatarajia moto huu kusambaa haraka kutokana na upepo mkali,” amesema Meya Bass, akisisitiza utabiri kwamba upepo utaongezeka kuanzia Alhamisi usiku hadi Ijumaa asubuhi.

Muujiza wa nyumba moja kusalimika

Wakati moto wa kutisha ukiwa umeshateketeza nyumba 10,000 Los Angeles, kuna muujiza wa nyumba moja katika mji wa Malibu iliyosalia salama.

Picha za kushangaza zilionyesha jinsi Malibu – paradiso ya pwani iliyokuwa nzuri siku chache zilizopita – ilivyoteketezwa kabisa na moto huo, huku mistari yake maarufu ya miti ya mitende ikibakia magogo meusi yaliyoungua.

Kiongozi wa Polisi wa Kaunti ya Los Angeles, Robert Luna, aliwaambia waandishi wa habari usiku wa jana kwamba idadi ya vifo ni 10, inatarajiwa kuongezeka.

“Inaonekana kama bomu la atomiki limeanguka kwenye maeneo haya. Sitarajii habari njema, na hatutarajii idadi nzuri,” amesema Luna, huku ripoti za vifo vya kusikitisha vya waliokwama zikionekana.

Miongoni mwa watu waliounguliwa na nyumba katika eneo la Pacific Palisades karibu na Malibu ni watu maarufu.

Nyumba za Paris Hilton, Anthony Hopkins, Tina Knowles, John Goodman, Candy Spelling, Milo Ventimiglia, na Miles Teller ziliteketezwa na moto huo.

Katika maeneo mengi ni mabaki ya msingi wa nyumba na mabomba ya moshi pekee yaliyosalia.

Moto wa Palisade mji ulioko kati ya Santa Monica na Malibu upande wa Magharibi wa Los Angeles na uliowaka  Eaton karibu na Pasadena Mashariki, tayari imetajwa kuwa mioto ya kihistoria iliyoleta uharibifu mkubwa zaidi katika historia ya Los Angeles.

Kushindwa kwa mifumo ya jiji hili lenye msimamo mkali wa kisiasa kusimamia moto huo kumewafanya wengi kuomba Meya Bass na Gavana Gavin Newsom wajiuzulu.

Rais Joe Biden, aliyetangaza hali ya maafa makubwa Jumanne ya Januari 7, aliahidi Serikali kuu italipia asilimia 100 ya gharama za ukarabati kwa siku 180 zijazo, ikiwa ni pamoja na kuondoa mabaki na nyenzo hatari, makazi ya muda na mishahara ya wahudumu wa dharura.

“Nimemwambia gavana na maofisa wa serikali za mitaa wasijali gharama kufanya wanachopaswa kufanya kudhibiti moto huu,” amesema Biden baada ya kukutana na washauri wakuu Ikulu ya White House.

Serikali bado haijatoa takwimu kuhusu gharama ya uharibifu, lakini mtabiri wa hali ya hewa wa kibinafsi, AccuWeather, amekadiria hasara ya kiuchumi kuwa kati ya Dola za Marekani bilioni 135 hadi 150.

Hii inaashiria changamoto kubwa ya ukarabati na ongezeko la gharama za bima ya nyumba kwa wamiliki wa mali.

“Tayari tunaangazia mpango wa kujenga upya jiji la Los Angeles kwa kasi,” amesema Meya wa Democrat, Karen Bass, ambaye amekosolewa vikali na Rais mteule Donald Trump, wanachama wa Republican na viongozi wa biashara wa Los Angeles kutokana na jinsi alivyoshughulikia janga hilo.

Anthony Mitchell (67) aliyekuwa mlemavu na mwanawe Justin, aliyekuwa na ugonjwa wa kupooza kwa ubongo (cerebral palsy), walikuwa wakisubiri gari la wagonjwa kuwachukua lakini hawakuweza kutoka, binti ya Mitchell, Hajime White, ameliambia The Washington Post.

Shari Shaw ameiambia tovuti ya KTLA kwamba alijaribu kumshawishi kaka yake, Victor Shaw mwenye umri wa miaka 66, kuondoka usiku wa Jumanne, lakini alikataa, akisema angepambana na moto huo.

Timu za uokoaji zilipata mwili wake akiwa na bomba la maji mkononi.

Moto ulivyokuwa ukisambaa

Kwa jumla, mioto mitano iliteketeza Kaunti ya Los Angeles ukiwamo moto wa Palisades uliodhibitiwa kwa asilimia sita pekee, moto wa Eaton ukiwa haujadhibitiwa kabisa. Anga ilikuwa imejaa ndege zinazomwaga maji na kemikali za kuzuia moto juu ya vilima vinavyowaka moto.

Alhamisi jioni, maofisa waliwahimiza zaidi watu kuzingatia amri za kuhama baada ya moto mpya kuibuka na kuenea kwa kasi.

Moto wa Kenneth umeteketeza kwa kasi eneo la West Hills kiasi cha wahudumu wa dharura 900 kuchoka na walihamishwa kutoka kwa maeneo mengine yenye moto mkali Kusini mwa California ili kulinda nyumba na kujaribu kudhibiti moto huo.

Moto huo ulianza alasiri katika Bonde la San Fernando, karibu kilomita 3.2 kutoka shule inayotumiwa kama makazi ya waathirika wa moto, kisha ukasambaa hadi Kaunti ya Ventura jioni.

Related Posts