Pamba yaleta beki la TP Mazembe

PAMBA Jiji ipo katika hatua za mwisho kumalizana na beki wa zamani TP Mazembe, Chongo Kabaso raia wa Zambia kuja kuimarisha safu yake ya ulinzi.

Pamba ambayo imepanda Ligi Kuu msimu huu, ni kama haijaanza vizuri kwani iko nafasi mbaya katika msimamo wa ligi kwani inashika nafasi ya 14.

Katika mechi 16 ilizocheza Pamba imefunga mabao manane na kuruhusu mabao 16, Huku matokeo hayo yakionyesha kuwa safu ya ulinzi ya kikosi hicho kuna mahali kinavuja. Baada ya mzunguko wa kwanza wa ligi kumalizika tu, mabosi wa klabu hiyo wakaamua kuziba mahali panapovuja, ikiwemo eneo la ulinzi.

Beki huyo (32) ambaye anaitumikia Kabwe Warrious kwa sasa, amekuwa akipata nafasi katika timu ya Taifa ya Zambia, huku ndani ya kikosi anachochezea hapati namba muda mwingi.

Mzambia huyo ambaye kama mazungumzo yao yatamalizika vyema basi atakuwa ndani ya Pamba, kwa sasa ni mchezaji huru baada ya kumaliza mkataba wake na Kabwe Desemba 2024.

Mwanaspoti linafahamu kuwa, Pamba iliamua kufanya uamuzi wa kumsajili beki huyo kutokana na matokeo mabaya ambayo wameyapata mzunguko uliopita. Taarifa za ndani zinasema: “Mipango ya timu sio kusajili tu beki. Tunaendelea kuimarisha kikosi, hivyo tukimaliza mazungumzo basi kila kitu kitakuwa sawa.”

Wakati huo huo, usajili wa Rally Bwalya bado haujaeleweka kufuatia klabu yake ya Napsa Stars ya Zambia kushindwa kutoa ushirikiano wa kumaliza dili hilo.

Mwanaspoti iliwahi kuandika juu ya dili la staa huyo wa zamani wa Simba, huku ikielezwa kuwa kiungo huyo alikuwa kwenye mazungumzo na Pamba.

Related Posts