Dar es Salaam. Mwanasiasa mkongwe, Dk Wilbroad Slaa (76) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kujibu shtaka la kusambaza taarifa za uongo kupitia mtandao wa X (zamani twitter).
Dk Slaa amefikishwa mahakamani hapo leo jioni, Januari 10, 2025 akikabiliwa na kesi ya jinai namba 993 ya mwaka 2025.
Dk Slaa aliyewahi kuwa balozi wa Tanzania nchini Sweden, alisomewa shtaka na Wakili wa Serikali, Clemence Kato anayeshirikiana na mawakili Tumaini Mafuru na Abdul Bundala.
Wakili Kato, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki amedai mshtakiwa anadaiwa kutenda kosa hilo chini ya kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015.
Amedai mshtakiwa alitenda kosa hilo Januari 9, 2025 ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikielezwa kupitia jukwaa la mtandao wa kijamii wa X katika akaunti ya Maria Sarungi @MariaSTsehai aliandika ujumbe uliosomeka:
“Wakubwa wametafutana, nikisema wakubwa namaanisha Mwamba na Samia, na wala hatuna maneno ya kumung’unya… na kimsingi wamekubaliana Suluhu Samia amekubali atatoa pesa, Suluhu Samia amekubali ataongeza nguvu ya pesa ni dhahiri atatoa pesa… hizo ni hela za Watanzania wanazichezea Samia na watu wake.”
Pia, anadaiwa kuandika: “Samia toka muda mrefu haangaikii tena maendeleo ya nchi anahangaikia namna ya kurudi Ikulu na namna yake ya kurudi Ikulu ni kwa njia hizo kama kumsaidia mtu kama Mbowe.”
Anadaiwa kuandika taarifa hizo akijua ni za uongo. Dk Slaa amekana kutenda kosa hilo.
Upande wa mashtaka umedai upelelezi haujakamilika na umeomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Upande wa utetezi ukiongozwa na wakili Hekima Mwasipu anayeshirikiana na Sanga Melikiori umedai shtaka linalomkabili lina dhamana, hivyo aliomba Mahakama itoe masharti nafuu ya dhamana.
“Tunaomba Mahakama yako itoe masharti nafuu ya dhamana dhidi ya mshtakiwa huyu ambayo hayatambana kufanya kazi zake au kutoka sehemu moja kwenda nyingine,” ameomba Mwasipu.
Upande wa mashtaka ulipinga ombi hilo ukidai umewasilisha mahakamani kiapo kuzuia dhamana ya mshtakiwa.
Wakili Kato amedai maombi hayo yameambatanishwa na kiapo kilichoandaliwa na mpelelezi wa kesi hiyo, SSP George Bagyemu.
“Kiapo hiki kimewasilishwa mahakamani hapa chini ya kifungu 148(b) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai( CPA) Sura ya 20 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022,” amesema.
Amesema kiapo cha kuzuia dhamana ya mshtakiwa kiliwasilishwa kupitia mfumo wa mtandao wa Mahakama.
Mawakili wa utetezi walipinga kiapo hicho wakidai hawajapatiwa nakala.
“Hatuna nakala ya maombi waliyowasilisha wenzetu kwa njia ya mtandao, hivyo tunaomba tupatiwe nakala hiyo,” ameomba Mwasipu akieleza wanaitaka waweze kujibu na kusikilizwa.
“Lakini kiapo hicho kwa nini wasitupatie na je, tuna uhakika gani kama kimesajiliwa kwenye mfumo wa Mahakama?” amehoji wakili Melikiori.
Hata hivyo, wakili Kato amedai taratibu zote za usajili wa maombi hayo na kiapo zimefuatwa, akieleza wanaweza kuingia kwenye mfumo kuangalia.
Hakimu Nyaki amesema maombi hayo yamewasilishwa kwa kushtukiza, hivyo yatajadiliwa Jumatatu, Januari 13, 2025.
“Kwa kuwa maombi haya mnetupatia kwa kutushtukiza, tutajadili kiapo hicho Jumatatu na mshtakiwa ataenda rumande hadi siku hiyo,” amesema.
Baada ya maelezo hayo, Dk Slaa amerudishwa rumande hadi Jumatatu.
Asubuhi ya leo kupitia mitandao ya jamii zilisambaa taarifa ikiwamo sauti ya Dk Slaa ikieleza amekamatwa na polisi na amepelekwa Kituo cha Mbweni, Dar es Salaam.
“Nawajulisha tu kwamba kuna polisi wamenifuata, nitawajulisha kitakachotokea. Napelekwa Mbweni kituoni,” alisikika Dk Slaa katika sauti hiyo.
Alipozungumza na Kituo cha Redio cha Wasafi FM Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alithibitisha kukamatwa na kushikiliwa Dk Slaa kwa mahojiano.
“Ni sahihi daktari yupo, tuko naye na tumekuwa na mahojiano naye kwa baadhi ya mambo na mahojiano yetu yanakwenda vizuri kwa hiyo tunaangalia mifumo ya kisheria inatuelekeza nini cha kufanya naamini taarifa zaidi zitatolewa baadaye,” alisema.
Dk Slaa aliwahi kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na mbunge wa Karatu.