Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa majaji wa Mahakama ya Rufani wanne.
Pia ameteua wenyeviti wa bodi na kumpangia kituo cha kazi balozi mmoja.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Januari 10, 2025 na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dk Moses Kusiluka walioteuliwa Latifa Alhinai Mansoor anayekuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani. Kabla ya uteuzi huo, alikuwa Jaji Mfawidhi, Kituo Jumuishi, Morogoro.
George Masaju ameteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani. Kabla ya uteuzi alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu na Mshauri wa Rais, Sheria.
Dk Deo Nangela ameteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, awali alikuwa Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Sumbawanga.
Mwingine aliyeteuliwa ni Dk Ubena Agatho anayekuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani. Kabla ya uteuzi alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Biashara, Dar es Salaam.
Katika hatua nyingine, Rais Samia amempangia kituo cha kazi nchini Brazil, Balozi Dk Stephen Simbachawene anayechukua nafasi ya Balozi Profesa Adelardus Kilangi ambaye amepangiwa majukumu mengine.
Rais Samia pia amemteua Uledi Mussa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kipindi cha pili.
Profesa Zacharia Mganilwa ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi wa Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE), akichukua nafasi ya Profesa Wineaster Anderson aliyemaliza muda wake.
Katibu Mkuu Kiongozi, Kusiluka katika taarifa hiyo iliyosainiwa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Sharifa Nyanga amesema majaji hao wataapishwa kwa tarehe itakayopangwa baadaye.