Sanga atua kwa mkopo Prisons

KIUNGO mshambuliaji, Rabbin Sanga, amekamilisha uhamisho wa mkopo wa miezi sita kujiunga na  Tanzania Prisons akitokea Singida Black Stars, hatua iliyofanywa na mabosi wa maafande hao kama sehemu ya mkakati wa kuimarisha kikosi chao kilichouanza vibaya msimu huu.

Tanzania Prisons ambayo ipo nafasi ya 13 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, imeshinda mechi tatu tu kati ya 16 na kutoa sare tano na kukumbana na kichapo katika michezo minane.

Uhamisho huu unampa fursa Rabbin ya kuonyesha makali yake kufuatia changamoto ya namba ambayo alikumbana nayo.

Rabbin, ambaye aliwahi kuitumikia Fountain Gates (Singida Big Stars/Singida Fountain Gates) katika timu za vijana na pia katika kikosi cha wakubwa, ni kiungo mwenye uwezo wa kuchezesha timu, hivyo anaweza kuongeza kitu kwenye eneo la kiungo cha maafande hao.

Huu ni uhamisho wa pili kwa Prisons kutoka Singida Black Stars, baada ya kiungo mkabaji Amade Momade (28) kujiunga na timu hiyo pia kwa mkopo.

Pamoja na Rabbin na Amade, Prisons pia imemsajili pia mshambuliaji mzoefu, Kelvin Sabato, ambaye ni mchezaji mwingine mpya anayeingia katika kikosi hicho kwa ajili ya kuimarisha safu yao ya ushambuliaji.

Related Posts