SERIKALI YATOA BILIONI 14.4 MRADI WA ENGARUKA

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo,akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika leo Januari 10,2025 katika tarafa ya Mtowambu wilayani Monduli.

Na.Mwandishi Wetu

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo, amesema Serikali imetoa shilingi bilioni 14.4 kwa ajili ya utelelezaji wa mradi wa magadi soda wa Engaruka na ulipaji fidia kwa wananchi waliopisha mradi huo.

Waziri Jafo,ameyasema hayo leo Januari 10,2025 wakati akizungumza kwenye mkutano wa hadhara katika tarafa ya Mtowambu wilayani Monduli.

Amesema kuwa wananchi 595 kutoka vijiji vinne vya Engaruka Chini, Mbaash, Idonyonado na Irerendeni watanufaika na fidia ya shilingi bilioni 6.2 huku fedha zingine zilizobaki zikienda katika shughuli mbalimbali za miradi ya maendeleo.

“Mradi huu wa magadi soda unaenda kuanza na mmepewa fidia hii kwaaajili ya kuanza mradi wake na shilingi bilioni 6.2 zinalipwa ili mradi uanze na sasa hivi zabuni zimeshatangazwa na tayari wawekezaji wameanza kuonesha nia ya kuwekeza kwenye mradi huu”.amesema Dkt.Jafo

Aidha Dkt. Jafo amesema fedha hizo zimetolewa na Serikali ikiwa ni mkakati wa kuendeleza miradi ya kimkakati yenye tija kwa Taifa.

Hata hivyo ameeleza kuwa, mradi huo ulikwama kutokana na changamoto za kimazingira katika Ziwa Natroni na kupelekea kuchelewesha mradi huo lakini Serikali ikafanya utafiti tena na kuja na maamuzi kutoka kwa wataalam na kuona eneo la vijiji vinne linafaa sana katika uchimbaji magadi hayo ambalo ni eneo la uwanda wa juu wa ziwa hilo lenye magadi soda ya kutosha.

Amesema kuwa Viwanda vingi nchini vinatumia magadi soda hayo na Tanzania ni waagizaji wakubwa wa magadi soda kutoka nchi za Boswana na maeneo mengine huku ikitumia fedha nyingi za kigeni kuagiza.

Pia ameongeza kuwa mradi huo unaenda kuhamisha fedha hizo badala ya kununua nje magadi hayo yatatokea eneo la Engaruka

“Niwashauri wananchi kuanza kufikiria kujenga hoteli na nyumba bora ili ziwe fursa kubwa zenye tija ikiwemo uchomaji nyama bora ili wawekezaji waje kula nyama na kula vyakula vinavyouzwa na wenteji wa maeneo haya.amesisitiza Dkt.Jafo

Amesema kuwa Fedha zimeshaingizwa kwa aajili ya ulipaji fidia kupitia akaunti ya NDC huku fedha nyingine zitatumika kuendeshea mradi huo.

Naye Naibu Waziri wa Madini, Mhe.Dkt.Stephen Kiruswa alisema mradi huo uwe ni chimbuko la mafanikio kwa wananchi wa wilaya ya Monduli na Longido kwani mradi huu ni mkubwa na unatija Kwa wananchi.

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dkt. Selemani Jafo,akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika leo Januari 10,2025 katika tarafa ya Mtowambu wilayani Monduli.

Related Posts