Slovakia yatishia kuikatia Ukraine misaada, kisa gesi ya Russia

Bratislava. Waziri Mkuu wa Slovakia, Robert Fico ameonya kwamba taifa lake huenda likaisitishia Ukraine misaada ya kifedha na kibinadamu baada ya kugomea ufufuaji wa mkataba wa bomba la usafirishaji wa gesi asilia kutoka Russia kwenda nchini kwake.

Kwa mujibu wa Reuters, Fico ametoa tishio hilo jana, muda mfupi baada ya mazungumzo na Kamishna wa Nishati wa Umoja wa Ulaya Dan Jorgensen.

Ametaja kitendo cha Ukraine kugomea ufufuaji wa mkataba wa bomba hilo uliokoma Desemba 31, 2024, kuwa kinalenga kuihujumu Slovakia ambayo kwa kiwango kikubwa inategemea gesi ya bei rahisi kutokea nchini Russia.

“Hakuna jambo lolote iwe sheria za Kimataifa ama vikwazo ambavyo vinaweza kuzuia usafirishaji wa gesi kupitia Ukraine,” Fico alimweleza mwandishi wa habari wa Reuters katika mkutano unaowakutanisha viongozi wa juu wa mataifa ya Ulaya jijini Brussels, Ubelgiji.

Slovakia ni miongoni mwa mataifa ambayo yanaonja joto ya jiwe baada ya uamuzi wa Ukraine kugomea ufufuaji wa mkataba wa bomba la gesi kutoka Russia kwenda mataifa ya Ulaya.

Kwa mujibu wa Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy, taifa hilo liligomea mkataba huo ambao ulikuwa unalipatia mamilioni ya dola, kwa sababu kufanya hivyo ni sawa na kufadhiri uvamizi wa Russia kwenye ardhi ya Ukraine.

Bomba hilo lilikuwa tegemeo kwa mataifa ya aya hususan ni Slovakia na Kosovo ambayo yalikuwa yakijipatia gesi asilia kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na viwandani kwa bei rahisi kutoka nchini Russia.

Kwa mujibu wa Fico, Slovakia itapoteza kiasi cha dola za Marekani 515 milioni kutokana na gharama za usafirishaji wa gesi hiyo kutoka mataifa mengine huku ikitarajia kupoteza hadi dola 1 bilioni kama ongezeko la fedha kwenye gharama ya kununua gesi hiyo.

“Endapo tatizo hili halitatatuliwa, Serikali ya Jamhuri ya Slovakia itachukua hatua madhubuti kukabiliana na Ukraine kwa siku zijazo,” alisema Fico.

Alitaja baadhi ya hatua hizo kuwa ni pamoja na kuhamasisha kura ya Veto katika Umoja wa Ulaya kuhusiana na masuala yote yanayohusiana na Ukraine hususan ni kura inayolenga kuiondolewa kwa misaada yote ya kifedha na kibinadamu kwa raia wa Ukraine.

Pia, alitishia kuwarejesha kwao, raia wa Ukraine ambao ni wakimbizi waliopewa hifadhi nchini humo, na kuikatia Ukraine nishati ya Umeme ambayo inanufaika nayo kutokea Slovakia.

Kauli hiyo ya Fico imekuja zikiwa zimepita siku chache tangu atembelee Russia na kufanya mazungumzo na Rais Vladimir Putin ambaye alimhakikishia kuwa taifa lake halina tatizo kuhusiana na ombi lake la kuendelea kunufaika na gesi yake.

Kikao cha Umoja wa Mataifa kilichotarajiwa kuketi kati ya wawakilishi wa Slovakia, Ukraine na Kamisheni ya Ulaya kujadili suala la gesi hiyo kiliahirishwa jana baada ya Ukraine kugoma na kusema haitoshiriki kikao hicho.

Hata hivyo, Slovakia na Kamisheni ya Ulaya ziliendelea kwa kuchukua hatua ya kuanzisha Kamati maalumu ya kufuatilia suala hilo, faida na hasara zake kwa wanachama wa Umoja wa Ulaya na kuangalia namna bora ya kutatua changamoto hiyo.

Waziri wa Mambo ya ndani wa Slovakia, Matus Sutaj Estok alikosoa msimamo huo wa Ukraine na kuuita usaliti kwa mataifa ya Ulaya yanayonufaika na gesi ya bei rahisi kutoka nchini Russia.

Estok alichapisha kauli hiyo aliyoiita Ukraine ni Msaliti katika akaunti yake ya Mtandao wa Facebook, naye akisisituiza kuwa Slovakia itasistisha misaada yake kwa Ukraine hususan ni ya kibinadamu, kijeshi na kifedha.

“Ukraine imesahau kuwa inapokea misaada lukuki kutoka Slovakia baada ya kugomea bomba la kutuletea gesi. Uamuzi wao huo unaashiria kuwa siyo tu wametusaliti lakini pia hawako na usawa inapotokea changamoto kwetu,” alisema.

Alisema Slovakia ilikuwa ikitarajia kuona huruma ya Ukraine kwenye suala la gesi hiyo.

Gesi asilia hiyo kutoka Russia ilikuwa ikisafirishwa kupitia bomba hilo kwenda mataifa ambayo ni pamoja na yale ya Umoja wa Ulaya, Austria, Italia, Kosovo na Slovakia.

Slovakia ndiyo itakayoathiriaka zaidi kutokana na mzozo huo kwa kuwa inategemea asilimia 60 ya gesi inayotumika nchini humo husafirishwa kutokea Russia.

Hadi leo, Ukraine haijatoa majibu wala kauli yoyote kuhusiana na kauli hiyo ya Fico.

Hata hivyo, Slovakia ilipotishia kukata umeme unaoelekezwa Ukraine wiki iliyopita, Waziri wa Nishati wa Ukraine, German Galushchenko alitoka hadharani na kusema haoni iwapo Slovakia itatekeleza suala hilo.

Wakati hayo yakiendelea, Ukraine imeendelea kuamini kuwa itapokea misaada ya mifumo ya Ulinzi wa anga, fedha makombora na ndege za kivita kutoka mataifa ya Ulaya.

Kwa mujibu wa Zelenskyy, mataifa hayo ya Ulaya yamemuahidi msaada wa kijeshi wenye thamani ya Dola za Marekani 2 bilioni na ongezeko la silaha za kivita ili kuiwezesha kupambana na hasimu wake Vladimir Putin wa Russia.

Zelenskyy alitoa kauli hiyo zikiwa zimebaki siku 10 hadi kuapishwa kwa Rais mteule wa Marekani, Donald Trump, ambaye amekuwa akikosoa misaada ya kijeshi inayotolewa na Marekani na mataifa ya Ulaya kwa Ukraine na kusema inaendelea kuchochea mzozo huo.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.

Related Posts