SMZ yajipanga kuwainua wakulima wa matango bahari

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wakubwa katika sekta ya uchumi wa buluu ili nao wawasaidie wafugaji wadogo wa matango bahari.

Amesema Serikali imeweka mkazo katika sekta tatu  katika uchumi wa buluu ambazo ni uvuvi, ukulima wa mwani na ufugaji wa mazao ya baharini, ukiwamo wa samaki, kaa, kamba  na matango bahari.

Dk Mwinyi amesema hayo leo Januari 10, 2025 alipozindua mradi wa Visiwani Sea Cucumber Farm uliopo Ukunjwi, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

“Lengo ni kuhakikisha wawekezaji wakubwa, wanawasaidia wafugaji wadogo kupata zana za kufanyia kazi na kuwapa vifaranga, hatimaye kununua mazao ya baharini kupitia wafugaji wadogo,” amesema.

Kwa upande mwingine, Rais Mwinyi ameeleza wawekezaji wakubwa katika sekta binafsi iwapo wataendelea na hatua waliyofikia katika ufugaji wa matango bahari, Zanzibar itakuwa kinara wa uzalishaji wake.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mwenyekiti wa Mradi wa Visiwani Sea Cucumber Farm Zanzibar, Toufiq Salim Turky amesema wanakusudia kujenga kiwanda cha kuchakata matango bahari Pemba.

Turky amesema lengo kuu ni kuwawezesha wananchi wengine kufuga ili kufikia lengo la kuzalisha tani 100 za matango bahari nchini.

Wakati huohuo, Dk Mwinyi amesema wazazi na walimu wana jukumu la kuwasimamia watoto kusoma kwa bidii baada ya Serikali kuandaa mazingira mazuri ya kusomea.

Ametoa kauli hiyo alipofungua shule mpya ya msingi ya Kojani, Wilaya Ndogo ya Kojani, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Dk Mwinyi amesema ujenzi wa shule unaofanywa na Serikali unalenga kuhakikisha watoto wanapata fursa nzuri ya elimu katika mazingira bora.

“Nafarijika kuona kuna usimamizi mzuri katika ujenzi wa shule hizi, sasa ni jukumu la wazazi na walimu kuwasimamia watoto wasome kwa bidii baada ya kuwekewa mazingira mazuri,” amesema.

Akizungumzia kuhusu ajira ameziagiza Wizara ya Afya, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali na Utumishi kuhakikish ajira zinapotolewa hususani Kojani ni lazima wapewe vijana wa kisiwa hicho. Amezitaka taasisi hizo kusimamia agizo hilo.

Agizo lingine amelitoa kwa Wizara ya Afya kupeleka boti moja ya matibabu Kojani, ikiwa ni miongoni mwa boti tano zilizoagizwa na wizara hiyo.

Amesema hatua hiyo itaongeza wepesi wa utoaji huduma kwa wananchi wa Kojani.

Rais Mwinyi amesisitiza kuwa, Serikali itaongeza wafanyakazi Kojani ili huduma ndogondogo katika nyanja mbalimbali zitolewe kisiwani hapo.

Akizungumzia michezo, amewahakikishia wananchi kuwa Serikali inakusudia kutoa upendeleo maalumu kwa kujenga kiwanja cha kisasa. Pia, ameahidi kujenga   hospitali ya wilaya kisiwani humo.

Kuhusu tatizo la maji ya bahari kuingia kwenye makazi ya wananchi, Dk Mwinyi ameahidi Serikali itakaa na wataalamu kulipatia ufumbuzi.

Awali, akitoa taarifa ya kitaalamu, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Khamis Abdalla Said amesema ujenzi wa shule hiyo umegharimu Sh5.382 bilioni ikiwa na madarasa 32, maabara, chumba cha kompyuta, maktaba na ukumbi wa kufanyia mitihani.

Shule hiyo ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 1,305 kwa mkondo mmoja.

Related Posts