Tanzania inathamini ushirikiano uliopo na Taifa la Marekani- Dkt. Mpango

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akifanya mazungumzo na Balozi wa Marekani nchini Tanzania anayemaliza muda wake Mhe. Michael Battle, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma leo tarehe 10 Januari 2025.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akisalimiana na Balozi wa Marekani nchini Tanzania anayemaliza muda wake Mhe. Michael Battle kabla ya mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma leo tarehe 10 Januari 2025.

MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema Tanzania inathamini ushirikiano uliopo na Taifa la Marekani ambao umetoa mchango katika maendeleo ya sekta mbalimbali.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akifanya mazungumzo ya kumuaga Balozi wa Marekani nchini Tanzania anayemaliza muda wake Mhe. Michael Battle, mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Chamwino mkoani Dodoma leo tarehe 10 Januari 2025. Amesema ushirikiano uliyopo umechagiza maendeleo katika sekta ya Afya ikiwemo mapambano dhidi ya UKIMWI kupitia Mfuko wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR), huduma za afya ya Mama na Mtoto pamoja na Programu ya M – Mama.

Makamu wa Rais amesema Tanzania inatarajia kuendeleza ushirikiano na Balozi ajaye wa Marekani katika maeneo mbalimbali kama vile kuongeza kiwango cha ufanyaji biashara pamoja na uanzishwaji wa usafiri wa ndege wa moja kwa moja kutoka Marekani hadi Tanzania ili kuvutia watalii.

Halikadhalika Makamu wa Rais amesema ushirikiano unahitajika zaidi katika masuala ya teknolojia kwa kutambua mchango wa Marekani katika ukuaji wa sekta hiyo duniani. Amesema teknolojia itawezesha kufanikisha azma ya serikali ya nishati safi ya kupikia na teknolojia ya kilimo itawezesha kuongeza uzalishaji na tija katika sekta hiyo.

Ameongeza kwamba, ni muhimu kuendeleza ushirikiano katika sekta ya elimu ikiwemo utoaji mafunzo kwa vijana na kuwajenga uwezo ili kuwa na rasilimali watu bora itakayosaidia kuharakisha maendeleo.

Makamu wa Rais amesema Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kufanya uchaguzi huru, wenye uwazi na amani ifikapo Oktoba mwaka huu.

Makamu wa Rais amempongeza Balozi Battle kwa kazi kubwa aliyofanya katika kipindi alichohudumu nchini ikiwemo ushirikiano katika vipindi vigumu kama vile wakati wa Janga la Uviko19.

Makamu wa Rais ametoa salamu za pole kufuatia kifo cha Rais wa 39 wa Marekani Hayati Jimmy Carter, ambapo amesema dunia imempoteza kinara wa demokrasia na amani. Aidha Makamu wa Rais ametoa salamu za pole kufuatia janga la moto lililotokea Los Angeles nchini Marekani na kupelekea kupoteza Maisha ya watu na mali zao.

Kwa upande wake Balozi wa Marekani anayemaliza muda wake Mhe. Micheal Battle ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushirikiano aliyopata na kuahidi Balozi ajaye ataendeleza mafanikio mbalimbali yaliyopatikana.

Balozi Battle amesema programu ya “R” Nne za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan sio tu muundo utakaoacha alama katika mageuzi ya maendeleo ya siasa nchini bali inatoa ushuhuda kwa dunia nzima namna taifa linavyoweza kufanya mageuzi ndani yake na kujenga utawala bora kwa lengo la kuwahudumia vema wananchi.

Imetolewa na

Ofisi ya Makamu wa Rais

10 Januari 2025

Chamwino, Dodoma.

Related Posts