Washington. Hukumu ya kesi iliyokuwa ikimkabili Rais mteule wa Marekani, Donald Trump imesomwa leo na kumfanya kuwa Rais wa kwanza wa Marekani kuhukumiwa kwa makosa ya uhalifu.
Pamoja na hukumu hiyo kutolewa leo Ijumaa Januari 10, 2025, Trump hatotumikia kifungo chochote wala kulipa faini katika shtaka la matumizi mabaya ya fedha kwa kumhonga mcheza picha za utupu ili asitoe taarifa za kushiriki ngono na mwanasiasa huyo.
Jaji wa Mahakama Kuu nchini humo, Juan Merchan amemsoma hukumu ya kesi hiyo ya Trump huku hukumu hiyo ikiwa haijaambatana na adhabu yoyote dhidi ya mwanasiasa na bilionea huyo.
Hukumu hiyo imesomwa siku moja tangu mawakili wa Trump wawasilishe ombi la kuitaka Mahakama hiyo ya Juu nchini Marekani kutosoma hukumu hadi Rais huyo mteule atakapoapishwa, ombi ambalo lilikataliwa.
Trump anatarajiwa kuapishwa Januari 20, 2025, kuanza kulitumikia taifa hilo akipokea kijiti kutoka kwa mtangulizi wake na Rais wa sasa wa taifa hilo, Joe Biden.
Aljazeera imeripoti kuwa, kutolewa kwa hukumu hiyo hakumnyimi Trump haki ya kuapishwa na kuingia Ikulu ya Washington kwa ajili ya kuanza kuwatumikia raia wa nchi hiyo.
Trump, ambaye amewahi kuiongoza Marekani kati ya mwaka 2017 hadi 2021, alikutwa na hatia kwenye makosa 34 ikiwemo kosa la kufanya ulaghai kwa nyaraka za kibiashara zinazohusisha malipo ya Dola za Marekani 130,000 kwenda kwa Stormy Daniels, ambaye ni mwigizaji wa picha za ngono nchini humo.
Trump amekuwa akikanusha madai hayo na kusema anatarajia kukata rufaa dhidi hukumu hiyo iliyosomwa leo baada ya kumtia hatiani
Huku akifuatilia kesi yake ndani ya Mahakama hiyo, Trump amesema mashtaka yaliyokuwa yakimkabili ni moja ya uzoefu mbaya aliowahi kukutana nao huku akisisitiza kuwa hajawahi kutenda uhalifu wowote.
“Nimekuwa nikiwindwa sana kisiasa,” Trump alieleza mbele ya Jaji ambaye amemsomea hukumu hiyo.
Pia, amesema waliomfungulia mashtaka hayo walikuwa na lengo na kuchafua taswira yake kwa umma ili asishinde uchaguzi, jambo ambalo amedai hawakufanikiwa na kamwe hawatofanikiwa.
Waendesha mashtaka jijini New York walikuwa wakidai kuwa malipo aliyofanya Trump dhidi ya mwigizaji huyo wa picha za ngono yalilenga kumnyamazisha asitoe ushirikiano dhidi ya mashauri ya unyanyasaji wa kingono yaliyokuwa yanamkabili.
Malipo hayo yanadaiwa kufanya na Trump mwaka 2016 wakati wa kampeni za uchaguzi Mkuu wa taifa hilo ambapo alishinda na kuwa Rais wa taifa hilo dhidi ya Mgombea wa Chama cha Democrats Hillary Clinton.
Trump, ambaye amekuwa akidai kutokuwa na hatia amekuwa akikanusha kila mara kufanya unyanyasaji wa kingono katika mahusiano aliyowahi kuwa nayo.
Mwandishi wa Al Jazeera, akiripoti kutokea Washington DC, Alan Fisher amesema waendesha mashtaka wa Serikali walikuwa wakiiomba Mahakama imhukumu na kumpa adhabu Trump.
Pia, jaji wa kesi hiyo amesema kuwa ilikuwa kesi ya aina yake na ngumu kuitolea uamuzi, hata hivyo hatma yake imefikiwa na Mahakama imemhukumu bila adhabu yoyote.
Katika Mahakama ya New York, chini ya Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Peanal Code) Mahakama itatoa hukumu isiyo na adhabu kwa mshtakiwa pale itakapobaini kuwa hakuna madhara endapo mshtakiwa aliyetiwa hatiani hana madhara hata asipofungwa jela ama kulipa faini.
“Tukio la leo lilikuwa la kushangaza na ninashukuru nalo limepita, tutakata rufaa dhidi ya hukumu hiyo ambayo haina faida yoyote na kurejesha İmani yetu kwa Wamarekani katika mfumo wetu wa kutoa haki,” ameandika Trump kwenye akaunti yake ya mtandao wa Truth.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.