Watendaji kwenye vituo vya kutolea huduma za afya waliopo kwenye Mkoa wa Manyara wamekumbushwa kuendelea na utaratibu wa kulipa madeni ya Bohari ya dawa (MSD) kwani kufanya hivyo ni kuiwezesha MSD kuwa na mtaji mzuri wa kuendelea kununua bidhaa za afya ambazo zinasambazwa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Manyara Dkt. Andrew Method alipokuwa anafungua kikao cha wadau na wateja wa MSD kanda ya Kilimanjaro wa mkoani wa Manyara.
Dkt. Method amewakumbusha watendaji hao kuwa ubora wa huduma za MSD tunazoziona leo kwenye vituo vya kutolea huduma za afya umechangiwa na upatikanaji mzuri wa fedha za kuiendesha MSD.
Pamoja na kulipa madeni yetu kwa MSD, lakini tuendelee kufanyakazi kwa ukaribu na taasisi yetu hii na pale penye changamoto basi ni vizuri tukakaa nao kutatua ili kuondoa malalamiko kwa wapokea huduma ambao ni wananchi alisema Dkt. Method.
Hata hivyo Dkt. Method ameipongeza MSD kwa kuboresha huduma kwa Mkoa wa Manyara ambapo huduma hizo zilizoboreshwa zimewezesha kuongezeka kwa upatikanaji wa bidhaa za afya hadi kufikia asilimia 95% .
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Dkt. Vicent Gyunda ambaye ni mshiriki wa kikoa hicho cha wadau amesema vikao hivi vinaisaidia MSD kwanza kupata mrejesho kutoka kwetu ambao ni wateja wao lakini vilevile vikao hivi vinasaidia kuongezeka kwa bidhaa za afya kwa asilimia 98% katika Wilaya ya Kiteto.