Dar es Salaam. Ubongo ni kati ya viungo muhimu katika mwili wa binadamu, ni chanzo kikuu cha kudhibiti mifumo yote ya mwili.
Wataalamu wa afya wamekuwa wakisisitiza juu ya umuhimu wa kulinda afya ya ubongo ili viungo vingine katika mwili wa binadamu viweze kufanya kazi vizuri.
Hata hivyo, kutokana na tabia pamoja na mambo mbalimbali yanayofanywa na binadamu, ama kwa kujua au kutojua, yanaweza kuathiri afya ya ubongo na kusababisha madhara kwa mwili mzima.
Wataalamu na maandiko mbalimbali ya afya yanabainisha baadhi ya mambo hayo kuwa ni kutopata muda wa kutosha wa kupumzika, kutozingatia ulaji wa lishe bora, kuwa na msongo wa mawazo kwa muda mrefu pamoja na matumizi ya vifaa vya kidijitali kama vile simu, televisheni kwa muda mrefu.
Akizungumza na Mwananchi, Mwanasaikolojia Modesta Kimonga anasema ili kuimarika kwa afya ya ubongo, binadamu anahitaji utulivu.
Kimonga anasema utulivu huo unapatikana kwa njia mbalimbali, ikiwemo kupata muda wa kutosha wa kupumzika, akisisitiza kuwa kitaalamu inashauriwa kulala kwa angalau saa 7 hadi 8 kwa mtu mzima.
“Mtu anapopata muda wa kutosha kulala inausaidia ubongo kuboresha utendaji kazi wake ambao unapelekea hata viungo na mifumo mingine nayo kufanya kazi kwa ufanisi unaotakiwa.
“Kutofanya hivyo kunaweza kusababisha mhusika kuhatarisha afya yake ya ubongo na hatimaye kusababisha changamoto mbalimbali kujitokeza, ikiwemo kumuweka katika hatari ya kupata kiharusi, kupungua kwa uwezo wa kumbukumbu na mengineyo,” anaeleza.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), msongo wa mawazo ni mvurugano katika akili hutokana na sababu kadhaa, kama vile mkwamo katika uhusiano, uchumi na mengineyo, huwakumba mtu mmoja kati ya wanne kwa nyakati tofauti.
Msaikolojia Kimonga anasema binadamu anapokuwa na mawazo sana mifumo katika mwili, ikiwemo utendaji kazi wa ubongo na hata mfumo wa kutengeneza homoni mbalimbali pia unaathirika.
“Msongo wa mawazo ni tatizo kubwa kwa sababu maisha ya binadamu na utendaji kazi wa mwili unategemea sana utimamu wa ubongo,” anasema.
Anaongeza kuwa pamoja na kuathiri ubongo, vilevile unaweza kumuweka katika hatari ya kupata magonjwa mbalimbali, ikiwemo shinikizo la damu pamoja na magonjwa ya afya ya akili.
Matumizi ya simu za mkononi, televisheni na vifaa vingine vya kidijitali kwa muda mrefu katika ulimwengu wa sasa, yanaendelea kuongezeka.
Ingawa teknolojia imeleta faida nyingi, matumizi ya simu za mkononi kwa muda mrefu yanaweza kuathiri afya ya ubongo.
Msaikolojia Kimonga anaeleza kuwa tafiti mbalimbali zinaonyesha kuwa matumizi ya vifaa hivyo kwa muda mrefu, yanapunguza uwezo wa ubongo kufanya kazi yake vyema.
“Ninashauri kwa ustawi wa afya ya ubongo wako ni vyema kuepuka matumizi ya vifaa hivyo kwa muda mrefu na hakikisha unapata mapumziko.”
Kwa upande wa watoto, miongozo WHO inabainisha kuwa mtoto wa chini ya miaka miwili haruhusiwi kabisa kuangalia televisheni au kutumia vifaa kama vile kompyuta mpakato, vishkwambi na vinginevyo.
“Kuanzia miaka mitano na kuendelea muda wa mtoto kutumia vifaa hivyo unaweza kuongezwa taratibu kadiri anavyozidi kukua, lakini kabla ya kufikisha miaka 18 mtoto hatakiwi kutumia vifaa hivyo kwa zaidi ya saa tatu,” anasema.
Hata hivyo, anaeleza kuwa wazazi wengi hawana uelewa juu ya hatari ya kuwaacha watoto kutumia muda mrefu vifaa hivyo na hivyo kuwaacha watoto wakivitumia bila uangalizi wa muda na hatimaye kuwaweka katika hatari ya kupata changamoto mbalimbali za kiafya.
Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na kupata maumivu ya kichwa, kuumwa macho pamoja na kutopata usingizi wa kutosha kutokana na kutumia muda mwingi kuangalia vifaa hivyo.
Kwa upande wa watoto, Daktari bingwa wa Fiziolojia ya homoni na mazoezi kutoka Chuo Kuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas) Fredrick Mashili, anaeleza kuwa mtoto kuangalia televisheni au vifaa hivyo vya kidijitali kwa muda mrefu kunaweza kumnyima fursa ya kuchangamana na watoto wenzake, jambo ambalo si jema kwa ustawi wa afya ya ubongo wake.
Matumizi ya pombe kupita kiasi na dawa za kulevya yanaathiri moja kwa moja afya ya ubongo.
Pombe inaweza kudhoofisha uwezo wa ubongo kuchakata habari, kuongeza hatari ya matatizo ya kumbukumbu na kudhoofisha michakato ya kimazingira ya utambuzi. Vilevile, dawa za kulevya husababisha mabadiliko katika kemia ya ubongo, yanayoweza kuathiri tabia na uwezo wa akili.
Pia tabia ya kupenda kukaa mpweke na kujitenga. Tovuti mbalimbali za afya zimeainisha namna tabia ya kupenda kukaa mpweke kwa kujitenga inavyoweza kuathiri utendaji kazi wa ubongo.
Kwa mujibu wa tovuti ya Premier Neurology &Wellness Center, tabia ya kutopenda kuchangamana na watu ina athari sawa na kutopata muda wa kutosha wa kulala katika ubongo.
Inafafanua kuwa mtu anapokuwa na tabia ya kupenda kuchangamana na watu mbalimbali katika jamii inasaidia kuuchangamsha ubongo na kuufanya uweze kujifunza mambo kwa haraka.
Vilevile inaeleza kuwa kuchangamana na watu pia inamsaidia mtu kuepukana na magonjwa mbalimbali yanayohusiana na afya ya akili, ikiwemo sonona pamoja na dementia.
Kwa upande wa watoto, Ofisa mkunga msaidizi kutoka Hospitali ya Wilaya ya Bahi, Anitha Mganga anasema tabia ya mzazi kumfungia mtoto na kumfanya kukosa fursa ya kuchangamana na wenzake inamnyima fursa ya kuchangamsha ubongo wake na kujifunza vitu vilivyopo katika mazingira.
“Kama mtoto mdogo hachezi na watoto wenzake yeye ni amefungiwa ndani tu hakuna wa kuongea naye mara kwa mara, muda wake mwingi anaangalia tu televisheni au kuchezea simu akiwa katika umri mdogo inaweza kumfanya kuchelewa kuongea,” anasema.
Pamoja na kupenda kujitenga, tabia ya kukaa eneo lisilo na mwanga wa kutosha kwa muda mrefu linatajwa pia kuwa na athari katika afya ya ubongo na huweza kusababisha mtu kupata changamoto mbalimbali za afya ya akili, ikiwemo sonona.
Tovuti hiyo inaeleza kuwa ili kuimarika kwa utendaji kazi na afya ya ubongo kwa jumla mtu anatakiwa kuhakikisha anakaa katika sehemu yenye mwanga na anapata mwanga wa kutosha wa jua.