UHONDO wa michuano ya Kombe la Mapinduzi 2025 hatua ya makundi inahitimishwa usiku wa leo kwa mchezo utakaowakutanisha wenyeji, Zanzibar Heroes dhidi ya Harambee Stars ya Kenya, ili kuamua timu ya kucheza fainali.
Jana usiku Burkina Faso iliyokuwa nafasi ya pili na pointi nne sawa na Kenya, ilikuwa ikimalizana na Kilimanjaro Stars ambayo inaburuza mkia na kupoteza tumaini la kucheza fainali Januari 13, huku Kenya ikiwa kileleni kwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufunga.
Wenyeji Zanzibar wenye pointi tatu wanahitaji ushindi ili kujihakikishia nafasi ya kucheza fainali Jumatatu dhidi ya Burkina Faso (kama jana imeshinda) au Harambee Stars, ilihali Wakenya wakihitaji japo sare tu wakate tiketi ya mchezo wa fainali ya michuano hiyo inayochezwa kwenye Uwanja wa Gombani, visiwani Pemba.
Mechi ya leo ni ngumu kutabirika kutokana na ushindani wa timu hizo mbili, kwani rekodi zinaonyesha katika mechi sita zilizopita tangu mwaka 2012 zilipokutana kwenye michuano ya Kombe la Chalenji, Kenya ilishinda mbili dhidi ya moja ya Zanzibar na michezo mitatu ilimalizika kwa sare.
Ushindi mkubwa baina ya timu hizo ni ule wa Novemba 27, 2015 wakati Zanzibar iliposhinda kwa mabao 3-1, ukiwa ndio pekee kwa timu hiyo ya visiwani dhidi ya Kenya, huku kipigo kikubwa ilichowahi kupewa na wapinzani wao hao ni kile cha 2-0 Desemba 3, 2013, huku mara mbili zilifungana mabao 2-2 na suluhu moja.
Kocha wa Zanzibar, Ali Suleiman Mtuli na Francis Kimanzi wa Harambee wameuzungumzia mchezo huo, kila mmoja akijinasibu ni mgumu.
Mtuli alisema kwa namna walivyoelekezana na kusahihisha makosa ya mechi iliyopita dhidi ya Burkina Faso walipolala 1-0, ana imani ya kupata matokeo ili kuwapa furaha mashabiki wanaotamani kuona kombe linabaki visiwani humo, huku Kimanzi alikiri licha ya ugumu wa wenyeji, kiu yao ni kufika fainali na kubeba taji.
“Tumerekebisha makosa ya mechi iliyopita, makosa madogo yalitugharimu. Haitakuwa mechi rahisi, lakini imani na morali ya wachezaji ni kupata ushindi na kwenda fainali,” alisema Mtuhi, huku Kimanzi akisema hawaoni cha kuwazuia kubeba ubingwa wa michuano hiyo ambayo kwa msimu huu inashirikisha timu za taifa.
Kenya, ilianza michuano hiyo kwa sare ya 1-1 na Burkina Faso kabla ya kuichapa Kilimanjaro Stars kwa mabao 2-0, huku Zanzibar ikiilaza Kilimanjaro kwa bao 1-0 na kulala 1-0 kwa Burkina Faso na kufanya timu hizo mbili za wageni kuwa kileleni, huku wenyeji Zanzibar wakifuata nafasi ya 3 na Tanzania Bara ikiburuza mkia.
Fainali ya michuano hiyo itakayochezwa Jumatatu, itashirikisha timu zitakazoshika nafasi mbili za juu.