Dodoma. Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amesema usaili wa walioomba ajira kwenye kada ya ualimu utafanyika kuanzia Januari 14 hadi Februari 24 mwaka huu kwenye vituo vya usaili vilivyopo kwenye mikoa ambayo wasailiwa hao wanaishi.
Simbachawene amesema nafasi za ualimu zilizotangazwa na Serikali ni 14,648 lakini walioomba ajira ni 201,707 hivyo wanatakiwa kuwapata wenye sifa ili wajaze nafasi hizo.
Simbachawene ametoa kauli hiyo leo Jumamosi, Januari 11, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za Wizara hiyo zilizopo Mtumba Jijini Dodoma.
Amesema kada hiyo hapo awali walikuwa wakipangwa moja kwa moja kwenye vituo vya kazi baada ya kupata ajira lakini sasa ni lazima wasailiwe ili wapate wenye sifa zinazohitajika kabla ya kupangiwa vituo vya kazi.
“Nafasi zilizotangazwa kujazwa kwenye kada ya ualimu zilikuwa ni 14,648 tu lakini mpaka sasa walioomba ajira kupitia Ajira Portal ni watu 201,707 utaona idadi ilivyo kubwa ya watu wanaohitaji kujaza nafasi hii lakini uhitaji wetu kwa sasa ni huo,” amesema Simbachawene.
Amesema usaili utafanyika kidijitali kwa wasailiwa ambao wamepewa namba maalum ya usaili kwenye vituo vilivyopo kwenye mikoa waliopo ili kupunguza gharama za usafiri kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine kwa ajili ya usaili huo.
Amewataka wasailiwa hao kufuata utaratibu uliopo wa kuomba ajira serikalini na kuachana na matapeli ambao hutumia nafasi hiyo kujipatia fedha kwa watu wanaoomba ajira serikalini.
“Ukiachana na wale ambao huwa wanatangaza kuwa wanatoa ajira na kumbe si kweli, kuna wale wengine ambao huwa wanajifanya wanatoka Tamisemi na mahali pengine kuwa wana uwezo wa kuwasaidia kupata ajira, niwaambie tu wasikubali kutapeliwa kwa sababu mchakato wa kupata ajira serikalini upo wazi na kila kitu kinaeleweka kwa sababu hakuna ubabaishaji,” amesema Simbachawene.
Amewataka wasailiwa ambao watapata nafasi hizo kuwa tayari kufanya kazi mkoa wowote watakaopangiwa na siyo kwenye mkoa anaoishi kwa kuwa nafasi hizo zimeombwa ili kupunguza tatizo la uhaba wa walimu nchini.
Waziri huyo amewataka wale watakaofanya usaili kwenda na vyeti vyao halisi vya kitaaluma, cheti cha kuzaliwa, kitambulisho ambacho kitamtambulisha msailiwa kama vile kitambulisho cha Taifa, kadi ya kupigia kura, leseni paspoti ya kusafiria au barua ya utambulisho kutoka kwenye mamlaka za serikali za mitaa.
Na kwa wale ambao vyeti vyao vya kitaaluma vina majina mawili huku kwenye kitambulisho cha Taifa na cheti cha kuzaliwa vina majina matatu waendesha na hati ya kiapo ya kumtambulisha kuwa ndiye yeye.
Simbachawene amesema mpaka sasa mchakato wa ajira serikalini umetoa kibali cha ajira takribani 155,008 kwenye kada mbalimbali nchini huku kada za afya na elimu ambazo walikuwa hawafanyiwi usaili hivi sasa wanafanyiwa ili kuwapata wale ambao wanakidhi vigezo.
Usaili wa ajira serikalini kwa njia ya mtandao ulizinduliwa rasmi Aprili mwaka 2024 ambapo utawawezesha wanaoomba ajira serikalini kufanya usaili kwenye vituo maalum vilivyopo kwenye mikoa yao na kupunguza gharama za malazi na kusafiri kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine tofauti na mfumo wa zamani ambao ulikuwa unawakosesha wengine nafasi ya kufanya usaili kwa sababu ya kukosa nauli na gharama za malazi kwenye mikoa waliokuwa wanafanyiwa usaili