AS Vita yabeba kiungo wa Coastal

AS Vita ya DR Congo imeendelea na operesheni ya kukusanya mastaa kutoka Bara baada ya kumnasa winga wa zamani wa Coastal Union, Dennis Modzaka.

Timu hiyo ipo chini ya kocha wa zamani wa Azam, Youssouf Dabo ikiendeshwa na matajiri wa Uturuki ikipiga hesabu za kusuka upya kikosi, huku kocha huyo akionyesha imani kubwa kwa wachezaji wa Tanzania.

Modzaka aliyeachana na Coastal baada ya kushindwa kuongeza mkataba, inaelezwa  ametua DR Congo kukamilisha uhamisho akiwa mchezaji huru.

Nyota huyo raia wa Ghana ni mchezaji wa tatu kutoka Tanzania aliyeivutia AS Vita baada ya mshambuliaji wa Mashujaa, Ismail Mgunda ambaye yupo kwenye mpango wa kusajiliwa na winga wa zamani wa Yanga, Msauzi Mahlatse Makudubela ‘Skudu.

Wachezaji hao wameshaanza mazoezi na kikosi hicho ambapo mabosi  wakijiridhisha watawapa mikataba. Mbali na Mgunda na Modzaka, pia Vita imempokea Skudu ambaye tayari ameshatua klabuni hapo akiendelea na mazoezi, ingawa haijaeleweka kama wote watapewa mikataba au la kwani kwa Mgunda inaelezwa ishu ya maslahi imeanza kuibua ugumu.

Mabingwa hao wa zamani wa DR Congo msimu huu walishindwa kufurukuta katika michuano ya CAF, baada ya kutolewa raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika na Stellenbosch ya Afrika Kusini, jambo lililowaamsha mabosi wa klabu hiyo kusuka kikosi imara ili kifanye kweli katika Ligi Kuu ya nchi hiyo.

Kiu ya Dabo ni kutaka kurejesha kile ilichokifanya timu hiyo 2018 ilipofika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika na kupoteza mbele ya Raja Casablanca ya Morocco. Timu hiyo pia ilicheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa kwa vipindi tofauti hivi karibuni kabla ya kuchemsha mapema msimu huu mbele ya Wasauzi.

Related Posts