KITENDO cha klabu ya AS Vita ya DR Congo kumnyemelea mchezaji Gibril Sillah, kimewafanya mabosi wa Azam FC kuwa na haraka ya kumwandalia ofa ya mkataba mpya nyota huyo kutoka Gambia, ambaye mkataba wake na timu hiyo ya Chamazi utamalizika mwishoni mwa msimu huu, Juni 2025.
Kwa mujibu wa taarifa za ndani, inaelezwa kuwa kocha wa zamani wa Azam, Youssouph Dabo, ambaye sasa anainoa AS Vita, amependekeza kusajiliwa kwa Sillah, ambaye msimu wa 2023/24 alifunga mabao manane kwenye Ligi Kuu ya Tanzania akiwa na timu hiyo.
Sillah, ambaye anajulikana kwa kasi na uwezo mkubwa wa kiufundi, msimu huu amefunga mabao matatu na ameendelea kuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha kocha wa sasa wa Azam, Rachid Taoussi ambacho kinaendelea kujifua kwa ajili ya duru la pili la Ligi Kuu tangu Januari 6 mwaka huu.
Chanzo cha ndani kimeeleza kuwa Azam inataka kumfunga kwa mkataba mpya Sillah mapema ili kumzuia kujiunga na AS Vita au klabu nyingine yoyote kubwa inayomhitaji.
“Mabosi wa Azam wanatambua umuhimu wa Sillah katika kikosi cha sasa na wanapanga kumwandalia ofa ya mkataba mpya. Hata hivyo, klabu inafanya kila liwezekanalo kuhakikisha inamlinda na kumzuia asiondoke, hasa kwa kuwa mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu huu,” kilisema chanzo hicho cha ndani.
Wakati huo huo, nyota wa zamani wa Azam, Kipre Tchetche, anayecheza katika klabu ya Kuching City ya Malaysia, amemtabiria makubwa beki ZouZou Landry aliyesajiliwa na Azam kuchukua nafasi ya Yannick Bangala, ambaye aliondoka klabuni hapo.
Kipre, akizungumza kuhusu Landry, alisema: “ZouZou Landry ni beki mwenye uwezo mkubwa. Ana nguvu, ufanisi na akili nzuri ya kimichezo. Nadhani atafanikiwa akiwa na Azam.”
Azam inapanga kumtoa kwa mkopo wa miezi sita kiungo Cheikhna Diakite kwa KMC ili ZouZou asajiliwe miongoni mwa nyota 12 wa kigeni wanaoruhusiwa kikanuni baada nafasi ya Bangala kuingizwa Alassane Diao.