UONGOZI wa Tabora United uko hatua za mwisho kukamilisha usajili wa aliyekuwa kipa wa Singida Black Stars, Fikirini Bakari kwa mkopo baada ya nyota huyo kuachana na Fountain Gate alikocheza kwa mkataba wa miezi sita.
Nyota huyo aliyekuwa akiichezea pia Fountain Gate kwa mkopo akitokea Singida, amepelekwa Tabora huku uongozi wa kikosi hicho wakimrejesha kipa mwenzake, Hussein Masalanga baada ya kuvutiwa na uwezo aliouonyesha tangu mwanzo mwa msimu huu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu Mkuu wa Tabora United, Adam Simba alisema usajili wowote utakapokamilika wataweka wazi ila kwa sasa hawezi kuzungumza lolote, hivyo tusubiri hadi muda muafaka utakapofika na mambo yote pia kukamilika.
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Singida Black Stars, Hussein Massanza alisema Masalanga amerejea baada ya kuichezea Tabora kwa mkopo wa miezi sita akieleza sababu ya kurudi ni kiwango alichokionyesha.
Kitendo hicho kinawafanya makipa hao kupishana ambapo Masalanga amerejea Singida Black Stars, huku Fikirini aliyeichezea Fountain Gate kwa mkopo akitolewa tena kwenda Tabora United. Kikosi hicho kimeondokewa na makipa wawili ambapo mbali na Masalanga, mwingine ni Mnigeria Victor Sochima aliyevunja mkataba.