Kesi iliyokuwa inamkabili Rais Mteule wa Marekani, Donald Trump imetolewa hukumu huku jaji aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, akimuachilia huru bila masharti na kumuepusha dhidi ya adhabu ya kifungo jela au kulipa faini, uamuzi uliozusha gumzo kubwa duniani kote.
Hukumu hiyo katika kesi ya matumizi haramu ya fedha, imetoka leo lakini jaji alikataa kutoa adhabu yoyote na kumuachilia huru kurejea Ikulu ya White House bila tishio la kifungo au faini.
Jaji wa Mahakama ya Manhattan, Juan Merchan angeweza kumhukumu Trump kifungo cha hadi miaka minne gerezani au kulipa faini lakini badala yake, alichagua adhabu ambayo iliepuka masuala magumu ya kikatiba kwa kumaliza kesi hiyo.
Katika kesi hiyo, Trump alikuwa akishtakiwa kwa kupotosha rekodi za biashara yake ili kuficha malipo ya dola 130,000 aliyoyafanya kwa mwigizaji wa filamu za maudhui ya kikubwa, Stormy Daniels.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Associated Press (AP), Trump bado anaweza kupiga kura baada ya hukumu hiyo lakini hataweza kumiliki bunduki na atabidi atoe sampuli za DNA.
Trump kwa kuwa alikutwa na hatia ya kupotosha rekodi za biashara, atakuwa na rekodi ya uhalifu mkubwa, jambo linaloathiri baadhi ya haki zake.
Kwa mujibu wa sheria za Marekani, watu waliokutwa na hatia ya uhalifu mkubwa hawaruhusiwi kumiliki silaha za moto na kila mtu aliyehukumiwa kwa uhalifu mkubwa, lazima atoe sampuli ya DNA kwa ajili ya hifadhi ya jinai ya serikali.