Bahi. Wananchi wapatao 18,604 wa Kata ya Chifutuka wameishukuru Serikali kwa hatua ya kuwaletea gari la kubebea wagonjwa ambalo litahudumu kwenye kituo cha afya Chifutuka ambacho pia kinahudumia wananchi kutoka Wilaya ya Singida Vijijini mkoa wa Singida.
Wakizungumza leo Jumamosi, Januari 11, 2025 wakati wa makabidhiano hayo na Mbunge wa wilaya ya Bahi Kenneth Nollo, wananchi hao wamesema msaada huo utawaondolea changamoto kubwa iliyowakabili kwa kipindi kirefu, hasa kwa wanawake wajawazito na wagonjwa wengine ya kukosa usafiri wa haraka ili kuokoa maisha yao pindi wanapoumwa.
Hussein Ilindilo mkazi wa kijiji cha Chifutuka ameishukuru Serikali kwa kuwaletea gari hiyo, kwani itasaidia kuokoa maisha ya wananchi hasa wanawake na watoto.
Ilindilo amesema kuwa yeye alinusuru maisha ya mke wake aliyekua mjamzito wakati huo kwa kukodi gari binafsi kwenda kutibiwa kwenye Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Dodoma kwa gharama ya Sh250,000.
“Siku za nyuma mke wangu alipata shida wakati wa kujifungua ilinilazimu nikodi gari kwa Sh 250,000 na ndio ilinisaidia kuokoa maisha ya mke wangu na hapo nilikua na hela ila nisingekua na pesa lolote lingeweza kutokea” amesema Ilindilo
Naye Isabela Paul, mkazi wa Chifutuka anayepatiwa matibabu katika hospitali ya Chifutuka kata ya Bahi, amesema anashukuru kwa uboreshwaji wa huduma za afya kwa kuwaletea madaktari bingwa na hivi leo wameletewa usafiri kwa wagonjwa na kusema gari hilo litasaidia sana kuokoa maisha ya wananchi.
Gari hilo litakwenda kusaidia kusafirisha wagonjwa pindi watakapokuwa na uhitaji wa rufaa kwenda hospitali ya wilaya au hospitali ya rufaa ya mkoa wa Dodoma.
Akizungumzia hilo Mganga Mkuu wa kituo cha Afya Chifutuka Dk Edson Luvakubusa ameeleza namna ambavyo huduma za upasuaji hasa kwa kinamama wakati wa kujifungua wanavyopata changamoto ya namna ya kuwapeleka hospitali za wilaya na mkoa ilivyokua tatizo.
“Hapo awali gari hadi lije walilisubiri umbali wa kilometa 130 kutoka wilayani Bahi hivyo ujio wa gari hilo la kubebea wagonjwa litasaidia kuokoa maisha ya wajawazito, na shughuli za upasuaji endapo mgonjwa atahitaji huduma zaidi, ” amesema.
Amesema kuwa gari hilo litaenda kuwa mwarobaini katika kuhakikisha linaokoa maisha ya wananchi
Akizungumza wakati wa kukabidhi gari hilo, Mbunge wa jimbo la Bahi Kenneth Nollo ametoa angalizo kwa watumishi na wananchi kutumia usafiri huo kwa uangalifu ili ulete tija kwa siku zijazo.
“Msitumie usafiri huu kupakia wake zenu au kupiga simu za dharura ili tuu uonekane wewe ni mtu wa kwanza kutumia gari hii haikubaliki na haileti maana” amesema Nollo.