Lyanga, Mashujaa kuna kitu Bara

UONGOZI wa Mashujaa FC unadaiwa upo katika mchakato wa kusaka saini ya mshambuliaji mkongwe Danny Lyanga anayekipiga JKT Tanzania, ili kuongeza nguvu kikosini kabla ya dirisha dogo la usajili kufungwa wiki ijayo.

Kama ambavyo Mwanaspoti liliripoti awali likimnukuu kocha Abdallah Mohamed ‘Bares’, akithibitisha uhitaji wa kusajili mshambuliaji, kiungo na beki mchakato huo umeanza kufanyiwa kazi.

Chanzo cha kuaminika kutoka Mashujaa kimeliambia Mwanaspoti kuwa uongozi umeanza mazungumzo na mshambuliaji huyo kwa ajili ya kumsajili ili aongeze nguvu eneo ushambuliaji.

“Ni kweli kuna mchakato unaendelea baina yetu na huyo mchezaji, mambo bado hayajakamilika. Mchakato ukiwa tayari kila kitu kitakuwa wazi kuhusu nafasi nyingine bado tunaendelea kufanyia kazi mapendekezo ya kocha,” kilisema chanzo.

“Hili ni dirisha la usajili mengi yatazungumzwa, yaliyo sahihi yatatolewa taarifa na uongozi mambo ya mitandaoni hatuyapi nafasi hii ni timu ambayo inafuata misingi na tupo tayari kutoa taarifa kwa wakati sahihi.”

Alipotafutwa Bares ili azungumzie mchakato huo, alisema kazi yake amemaliza anachosubiri ni kuletewa wachezaji ili waweze kujenga timu shindani.

“Mimi nimekabidhi ripoti kwa viongozi nimewaachia wafanyie kazi hhivyo kuhusu nani na nani wameongezwa nawaachia wao watatoa taarifa na kuweka wazi kinachoendelea,” alisema

Lyanga aliyecheza Tanzania Prisons, Geita Gold, Azam FC, Simba, Fanja amebakiza miezi sita kuendelea kuitumikia JKT Tanzania, hivyo ni ruhusa kwake kuzungumza na timu yoyote.

Related Posts