BEKI wa Simba, Che Malone Fondoh, amezua jambo klabuni Msimbazi ambako mabosi wa klabu hiyo wamegawanyika pande mbili kuhusu ishu yake.
Staa huyo raia wa Cameroon alikuwa na msimu bora sana wa kwanza, lakini sasa msimu huu baada ya makosa ambayo ameyafanya katika baadhi ya mechi, mabosi wa klabu hiyo wamemkalia vikao.
Mabosi wa Simba wamegawanyika kwa sasa kuhusu beki huyo, ambaye walimuita mezani kwa nia ya kuanza mazungumzo ya kumuongezea mkataba mpya.
Mkataba wa sasa wa Simba na beki huyo Mcameroon utafikia tamati mwisho wa msimu huu na baada ya kumalizika kwa msimu uliopita, Simba ilimweka katika orodha ya wachezaji watakaongezewa mapema mikataba yao ya kuitumikia timu hiyo.
Hata hivyo, makosa ambayo beki huyo ameyafanya katika baadhi ya michezo ya Simba msimu huu yameushtua uongozi wa timu hiyo ambao kwa sasa umeamua kusimamisha kwanza mpango huo wa kumuongezea mkataba mpya ili wajadiliane kwa kina kupata muafaka mmoja.
Habari ambazo Mwanaspotui limezipata kutoka kwa mmoja wa vigogo wa juu wa Simba zimefichua kuwa, kumekuwa na mgawanyiko wa mitazamo baina ya uongozi huo kuhusu beki huyo waliyemsajili mwaka 2023 akitokea Coton Sports ya kwao Cameroon.
“Baadhi ya viongozi wako tayari tumuongezee mkataba mpya Che Malone na kuna wengine wanaona tusiwe na haraka ya kufanya, hivyo na tumuangalie katika mechi zilizobakia za kumalizia msimu. Hapa katikati amekuwa na makosa mengi ambayo yanawapa wasiwasi maana yamekuwa yakiigharimu timu,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:
“Hivyo suala lake bado liko fifte fifte, iwapo akiendelea kufanya makosa uwanjani na tukafanikiwa kupata mchezaji mwenye kiwango na ubora kama alionao au zaidi, lolote linaweza kutokea.”
Tangu alipotua Msimbazi, Che Malone amekuwa mchezaji tegemeo wa kikosi hicho katika nafasi ya beki wa kati akitumika zaidi katika kikosi cha kwanza chini ya makocha tofauti.
Msimu wa kwanza alikuwa akiunda pacha na beki Mkongomani Henock Inonga aliyetimkia FAR Rabat ya Morocco baada ya msimu kumalizika na hivi sasa amekuwa akicheza sambamba na Abdulrazack Hamza na wakati mwingine akicheza na Chamou Karaboue.