KOCHA mpya wa Fountain Gate, Mkenya Robert Matano amewaahidi mashabiki na viongozi kutegemea mambo makubwa ndani ya timu hiyo, huku jambo kubwa analotaka ni sapoti ili wafanye vizuri katika mashindano mbalimbali.
Matano aliyekuwa anakifundisha kikosi cha Sofapaka nchini Kenya, alitangazwa kuifundisha timu hiyo juzi akichukua mikoba ya Mohamed Muya aliyetimuliwa Desemba 29, mwaka jana muda mfupi baada ya kichapo cha mabao 5-0 kutoka kwa Yanga.
Akizungumza na Mwanaspoti jijini Dar es Salaam, Matano alisema ni fahari kubwa kwake kupata nafasi ya kukiongoza kikosi hicho, licha ya kukiri kwamba haitakuwa rahisi kutokana na ushindani wa Ligi Kuu Bara kwa jinsi ambavyo amekuwa akiifuatilia.
“Unapotaja miongoni mwa Ligi bora hutoacha kuitaja ya Tanzania, nafurahia nafasi niliyopata hapa kwa sababu kwangu ni heshima, nimekuwa na mazungumzo chanya na viongozi wangu hivyo, tusubiri kuona kile kitakachotokea msimu huu,” alisema.
Hata hivyo, Mwanaspoti lilitaka kujua sababu ya Matano kuikataa Coastal Union licha ya kutua nchini mwanzoni mwa msimu huu na kufanya mazungumzo, ingawa hakutaka kuweka wazi zaidi ya kueleza anafikiria maisha yake mapya na Fountain Gate.
Kocha huyo anayefahamika kwa jina la utani la ‘Special One’, alijiunga na Sofapaka msimu huu baada ya mkataba wake na Tusker FC aliyoingoza kwa miaka sita kuanzia mwaka 2018 kumalizika, huku akitwaa ubingwa wa Kenya msimu wa 2021-2022.
Matano aliyewahi kuzifundisha timu mbalimbali zikiwemo za AFC Leopards na Ulinzi Stars, ameiongoza Sofapaka katika jumla ya michezo 15, ya Ligi ya Kenya huku akishinda mitano, sare sita na kupoteza minne akiiacha nafasi ya saba na pointi 21.
Katika kipindi chake cha ukocha kocha huyo, amewahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) mara nne akifanya hivyo na Sofapaka FC mwaka 2009 ambayo ameshaachana nayo msimu huu na Tusker FC kuanzia msimu wa 2012, 2020-2021, na 2021-2022.
Matano aliyewahi kutwaa tuzo ya kocha bora wa Kenya katima msimu wa 2009, 2020 na 2021, enzi za uchezaji wake alikuwa ni beki huku akizichezea timu mbalimbali zikiwemo za Abeingo, Nakuru Youth Olympic, Hakati FC, Kenatco FC kisha AFC Leopards FC.
Baada ya kucheza soka kwa takribani miaka 10, Matano alianza kazi ya ukocha akianzia kuifundisha Pumwani Sportif 1986.