Same. Mawasiliano barabara kuu ya Same -Mkomazi, wilayani Same yamerejea baada ya ujenzi wa Daraja la Mpirani kukamilika.
Daraja hilo ambalo lipo Kata ya Maore, lilivunjika Januari 2, 2025 baada ya nguzo zilizokuwa zimelishikilia kuathiriwa na mvua. Kuvunjika kwa daraja hilo kulisababisha adha ya usafiri na usafirishaji hasa kwa wananchi wanaoishi katika safu za milima ya Upare.
Januari 4, 2025 Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega akiwa ziarani wilayani Same, alipita kukagua ujenzi wa daraja hilo na akaagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuhakikisha ujenzi wa daraja hilo unakamilika ndani ya siku tatu.
Akizungumzia kukamilika kwa daraja hilo, Meneja wa Tanroads Mkoa wa Kilimanjaro, Motta Kyando amesema daraja hilo limeanza kutumika Januari 10, 2025 na huduma zote za barabara zinaendelea kama kawaida.
“Daraja limekamilika kwa asilimia 98 na limeanza kutumika tangu jana jioni, tunaishukuru Serikali kwa kuhakikisha wananchi wa maeneo haya wanaendelea na shughuli zao kama kawaida, kwa sasa magari yanapita kama kawaida,” amesema.
Diwani wa Maore, Rashid Juma amesema daraja hilo limeanza kupitika Januari 10 jioni. Amewashukuru wataalamu wa Tanroads kwa kazi kubwa waliyoifanya usiku na mchana kuwezesha mawasiliano ya barabara kujerea kama kawaida.
“Daraja limefunguliwa jana jioni na magari yameanza kupita, tunaishukuru Serikali na wataalamu waliokuwa wakifanya kazi hapa, maana kazi haikuwa ndogo lakini walikimbizana usiku na mchana, kuhakikisha linakamilika na mawasiliano ya barabara hii yanarudi, wananchi wanaendelea na shughuli zao za usafiri na usafirishaji kama kawaida,” amesema.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wananchi wa Kata ya Mpirani, wameishukuru Serikali kwa kukamilisha ujenzi.
Salim Kayanda, mkazi wa Kijiji cha Mpirani amesema kukamilika kwa daraja hilo ni fursa kwa wananchi wa ukanda wa milimani ambao wamekuwa wakijishughulisha na kilimo cha tangawizi.