Dar es Salaam. Mwanafunzi wa mwaka wa kwanza, Chuo cha Usimamizi wa Fedha( IFM) Sadik Mbelwa(20) amefikishwa katika Mahakama ya Mwanzo Kariakoo, kujibu shtaka la wizi wa simu na kompyuta, vyote vikiwa na thamani ya Sh1 milioni.
Mwanafunzi huyo anadaiwa kuiba vitu hivyo katika hosteli za Greenlight zinazomilikiwa na Chuo cha Teknolojia Dar es Salam (DIT).
Mshtakiwa huyo ambaye anachukua kozi ya kodi (Taxation) ngazi ya cheti hapo IFM, amefikishwa Mahakama hapo jana Ijumaa, Januari 10, 2025 na kusomewa shtaka linalomkabili.
Mbelwa alisomewa shitaka lake na karani wa Mahakama hiyo, Aurelia Bahati, mbele ye Hakimu Gladness Njau.
Bahati amedai kuwa mshtakiwa huyo anakabiliwa na kesi ya jinai namba 8 ya mwaka 2025.
Karani huyo amedai kuwa mshtakiwa huyo ameshtakiwa chini ya kifungo 258 na 265 cha Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Akimsomea shtaka lake, alidai kuwa mshtakiwa anadaiwa Desemba 11, 2024 saa 2:45 usiku maeneo ya Kisutu, kata ya Kisutu, kwenye hosteli za Greenlight zinazomililiwa na chuo cha Teknolojia Dar es Salaam (DIT) aliiba simu moja aina ya Sumsing Galaxy M21 yenye thamani ya Sh520,000.
Pia anadaiwa kuiba kompyuta mpakato moja aina ya HP yenye thamani ya Sh500,000 zote mali ya Joel Mdoe na Kelvin Philipo.
Mshtakiwa baada ya kusomewa shtaka lake, alikana kutenda kosa hilo.
Hakimu Njau alitoa masharti ya dhamana dhidi ya mshtakiwa huyo kuwa anatakiwa awe na mdhamini mmoja mwenyewe utambulisho unaotambulika kisheria atakaye saini bondi ya Sh500,000.
Mshtakiwa ameshindwa kutimiza masharti ya dhamana na amerudishwa rumande hadi Januari 16, 2025 kwa ajili ya usikilizwaji.