RAIS SAMIA ATOA AJIRA ZA WALIMU 14,648 KUPUNGUZA UHABA WA WALIMU NCHINI.

Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma

Imeelezwa Kuwa Kuanzia tarehe 14 Januari hadi terehe 24 Februari, 2025, usaili wa kada za Ualimu utaendeshwa na Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais (UTUMISHI); Ofisi ya Rais (TAMISEMI); Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia; Wizara ya Afya; Tume ya Utumishi wa Walimu; Ofisi za Wakuu wa Mikoa yote na wataalamu mbalimbali kutoka katika Taasisi za Umma.

Hayo yamebainishwa leo jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene katika mkutano na wanahabari ofisini kwake Mtumba.

Simbachawene amesema usaili huo una lengo la kujaza nafasi elfu kumi na nne mia sita na arobaini na nane (14,648) zilizotolewa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa lengo la kupunguza uhaba wa walimu nchini.

“Ninapenda kuchukua nafasi hii kuwasihi sana wale wote walioitwa kwenye usaili wajiandae vyema kwa usaili huo kwani nafasi hizi ni za ushindani.”

Waziri huyo amesema kulingana na mahitaji ya elimu kwa sasa, wataajiriwa wataalamu wa fani za Amali.

“Hivyo, nawasihi sana wale wote watakaopata nafasi ya kuajiriwa, wawe tayari kujiendeleza ili kuweza kukidhi matakwa ya ajira zao katika Utumishi wa Umma.”

Simbachawene amesema kuwa Usaili huo wa kada za Ualimu utafanyika katika Mkoa ambao kila msailiwa anaishi au aliombea kazi, Lengo kuu la utaratibu huo ni kuwapunguzia gharama za kusafiri na mambo mengine.

Sekretarieti ya Ajira ilitoa matangazo kumtaka kila msailiwa kuhuisha taarifa zake katika akaunti yake ya Ajira Portal sehemu iliyoandikwa ‘current physical adress’ kwani ndipo walipopanguwa vituo vya usaili kulingana na anuani walizojaza.

“Hivyo, ninawasihi sana waombaji wote kuhakikisha kila mmoja anakwenda katika kituo ambacho amepangiwa kwa ajili ya usaili kwani mahitaji yake ya msingi yapo huko.”

Aidha Simbachawene amesema usaili wa awali wa kuandika (Mchujo) kwa kada za Ualimu utafanyika kwa njia ya kuandika kwa mkono kwa kada zote na ngazi zote za elimu.

Hata hivyo Simbachawene amewakumbusha wale wote watakaokwenda kwenye usaili wahakikishe wanabeba vyeti vyao Halisi kikiwemo Cheti cha Taaluma na Cheti cha kuzaliwa.

Vilevile, wasailiwa wanapaswa kwenda na namba zao za usaili walizotumiwa kwenye akaunti zao za ajira portal pamoja na kuzingatia Ratiba kama ilivyopangwa na Sekretarieti ya Ajira.

“Kwa wale ambao kwenye vyeti vyao vya kitaaluma wanatumia majina mawili wakati kwenye cheti cha kuzaliwa na kitambulisho cha NIDA kuna majina matatu (3), au wale ambao majina yanatofautiana katika vyeti, wanapaswa kuwa na hati za kiapo (Affidavit au Deed Poll) ili kuthibitisha majina yao na vyeti husika.”




Related Posts