Arusha. Katika kukuza utalii wa matibabu na kufikia malengo ya kitaifa ya kutokomeza vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua, Serikali inatarajia kuanza kuwasomesha wauguzi na wakunga katika masomo ya ubingwa na ubingwa bobezi. Hayo yamesemwa leo Januari 11,2025 jijini Arusha na Waziri wa Afya Jenista Mhagama wakati akikagua na kuzindua chumba cha huduma za dharura kwa watu maalum ndani ya Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru.
Waziri Mhagama amesema kuwa serikali kupitia mfuko wa ‘Samia Super-Specialized scholarship Programme’ imekuwa ikitoa nafasi za ufadhili wa masomo ya ubingwa na ubingwa bobezi kila mwaka lakini wauguzi na wakunga wamekuwa nyuma.
Kwa msimu wa mwaka wa fedha 2023/2024 mfuko huo ulitengewa zaidi ya Sh10.9 bilioni kufadhili masomo ya madaktari 1,109 masomo ya ubingwa na ubingwa bobezi.
“Kwa kuwa Rais wetu (Dk Samia Suluhu Hassan amekuwa akitoa fedha hizi kila mwaka na mwaka huu ameahidi pia atatoa fedha zingine, basi Katibu Mkuu nakuagiza hakikisha mpeleke seti ambayo itajumuisha wauguzi na wakunga, ili nao wapate nafasi ya kwenda kusoma masomo ya ubingwa na ubingwa bobezi msimu wa mwaka huu 2025/2026 kwa sababu muda unaruhusu” amesema Mhagama.
Amesema lengo la nchi kuwa na wakunga na wauguzi wabobezi, mbali na kusaidia nchi kufikia malengo ya kitaifa ya kutokomeza vifo vya wajawazito wakati wa kujifungua, lakini pia itakuza utalii wa tiba kwa kuwaleta watu kutoka mataifa mbalimbali kuja kutibiwa hapa nchini.
Mbali na hilo, Waziri Mhagama ameipongeza Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru kwa kuanzisha huduma hiyo ya dharura wa watu maalum, ambayo itahudumia watalii wanaokuja Arusha lakini pia viongozi wa Serikali na sekta mbalimbali katika nchi za Afrika mashariki.
“Moja ya maeneo ya mkakati katika wizara yangu ni kukuza utalii wa tiba hasa kipindi hiki tunapoelekea kupokea ugeni mkubwa wa mashindano ya Afcon, hivyo tumeanza mazungumzo tena na serikali ya Cuba na wamekubali kuja kushirikiana nasi kutoa elimu ya utoaji wa huduma za dharura katika masomo ya ubingwa na ubingwa bobezi katika chuo chetu cha tiba cha Muhimbili,” amesema.
Awali, Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Mount Meru, Dk Alex Ernest amesema kuwa wameamua kuanzisha huduma hiyo baada ya kuona uhitaji hasa viongozi na watalii wanaohudhuria hospitalini hapo kutibiwa.
“Lengo ni kuhakikisha tunakuza utalii wa tiba kwa kuhakikisha watalii na viongozi mbalimbali wa heshima wanaokumbwa na matatizo ya kiafya hawasafirishwi kwenda mbali bali wanatibiwa katika hospital hiyo ili pia kuongeza mapato ya Serikali” amesema.
Amesema kuwa kuimarika kwa huduma za tiba katika hospital hiyo imesaidia kukuza mapato kila mwaka hadi kufikia Sh10.61 bilioni kwa mwaka 2023/2024 kutoka Sh7.11bilion walizokusanya mwaka 2022/2023.
Amesema kuwa hospitali hiyo yenye uwezo wa kuhudumia watu milioni 2.3 kwa mwaka ina wahudumu zaidi ya 300 wakiwemo madaktari na wauguzi lakini bado ina changamoto ya watumishi 162.
“Pia tunahitaji zaidi ya Sh14.8 kwa ajili ya kujenga jengo la wagonjwa wa nje (OPD) sambamba na mashine ya MRI” amesema Dk Ernest.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha Paul Makonda amewataka wahudumu wa afya nchini kutoa huduma kwa kuzingatia maadili ya kazi yao.