Seoul. Uchunguzi umebaini kuwa vifaa vya kurekodi taarifa ya mwenendo wa ndege ya Shirika la Jeju nchini Korea Kusini, viliacha kufanya kazi dakika nne kabla ya ndege hiyo kupata ajali na kulipuka.
Ndege hiyo aina ya Boeing 737-800, ikitokea Bangkok Thailand kwenda Muan nchini Korea Kusini ilikuwa imebeba abiria 181 wakiwemo abiria 175 na wahudumu sita, kati yao watu 179 wakiwemo wahudumu walifariki huku wahudumu wawili wakinusurika.
Tovuti ya The Guardina imeripoti leo kuwa kabla ya kulipuka ndege hiyo Desemba 29, 2024, ilipata hitilafu katika mfumo wa gia ya kutua kisha kutua kwa kutumia sehemu ya tumbo (uvungu) wa ndege hiyo.
Baada ya hapo iligonga nguzo zilizokuwa zimejengwa mwishoni mwa njia ya kurukia katika uwanja huo.
Maofisa wanaitazama ajali hiyo kama ajali hatari zaidi ya ndege kuwahi kutokea nchini Korea Kusini katika kipindi cha miaka 30 iliyopita, huku wakiwa na matumaini kuwa sanduku la kurekodi taarifa za mwenendo wa ndege hiyo lingeweza kuanika chanzo cha ajali hiyo.
Hata hivyo, Wizara ya Usafirishaji ya Korea Kusini imetoa taarifa kwa umma leo Jumamosi Januari 11,2025, kuwa kifaa cha kurekodi taarifa za ndege maarufu kama Flight Data Recorder (FDR) na kifaa maalum cha kurekodi sauti za wahudumu, abiria na marubani maarufu kama Cockpit Voice Recorder (CVR) vilikoma kufanya kazi dakika nne kabla ya ndege hiyo kupata ajali.
Katika taarifa hiyo, wizara hiyo ilisema kuwa hadi sasa haijabainika sababu gani ilichangia vifaa hivyo kuacha kufanya kazi na kuahidi kufanya uchunguzi kubaini chanzo cha tatizo hilo.
“Taarifa za CVR na FDR ni za muhimu katika uchunguzi wa tukio lolote la ajali ya ndege ila uchunguzi wowote hufanyika kwa kuzingatia uchambuzi wa taarifa mbalimbali hivyo tutafanya kila liwezekanalo kubaini chanzo cha ajali hii,” imesema wizara hiyo.
Wizara hiyo imesema kifaa cha CVR kilikuwa cha kwanza kufanyiwa tathmini kisha kusafirishwa kwenda nchini Marekani kwa tathmini na uchunguzi zaidi.
Pia imesema kifaa cha FDR, ambacho kilikuwa kimeharibiwa vibaya kutokana na kukosa kiunganishi kilipelekwa ilipo Ofisi ya Bodi ya Usafirishaji ya Taifa nchini Marekani wiki iliyopita kufanyiwa uchunguzi, baada ya Mamlaka nchini Korea Kusini kushindwa kuchota taarifa kutoka ndani yake.
Ajali hiyo ya kwanza kusababisha madhara kwa abiria tangu mwaka 1997, ndege ya Shirika la Korean aina ya Boeing 747 ilipopata ajali katika msitu wa Guam na kusababisha vifo vya watu wote 228 waliokuwemo.
Hadi sasa haijafahamika nini kilisababisha ndege hiyo kupata ajali hiyo. Uchunguzi huo unatarajiwa kuchukua hadi miezi kadhaa kabla ya kubaini chanzo halisi cha ajali hiyo.
Kipande cha video kilichosambaa kwenye mitandao ya kijamii kinaionyesha ndege hiyo ikiwa imeshindwa kuchomoa gia zote za kutua na kisha kugonga nguzo.
Kabla ya ajali hiyo, rubani alisikika akitoa taarifa ya dharura ya kwamba ndege hiyo imegongwa na ndege pori, huku akisema inatua ardhini kwa dharura kabla ya kushindwa kuchomoa gia hiyo ya kutua na kugonga nguzo kisha kulipuka.
Jeshi la Polisi nchini Korea Kusini lilivamia Ofisi za Shirika la ndege la Jeju na kuchukua nyaraka katika kile ambacho lilidai ni kufanya uchunguzi binafsi kubaini chanzo cha ajali, huku likiahidi kuchukua hatua za kisheria endapo kutabainika kufanyika uzembe wa aina yoyote.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.