Dar es Salaam. Diwani mstaafu wa Kiromo, Wilaya ya Bagamoyo, Mkoa wa Pwani (CCM), Hassan Usinga maarufu Wembe, amejitokeza kumwomba radhi waziri mwandamizi wa zamani, Dk Shukuru Kawambwa kwa kumdhalilisha.
Wembe ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Halmashauri ya Bagamoyo amesema kilichofanyika ni mambo ya kisiasa na anajutia uamuzi wake huo.
Tukio hilo lilitokea mchana wa Aprili 24, 2024 Kitongoji cha Kitopeni B wilayani Bagamoyo. Kipande cha video jongefu kilichosambaa mitandaoni kilimwonyesha Dk Kawambwa akishambuliwa kwa maneno makali na ya dharau akiwa na wenzake huku watu hao wakitaka waziri huyo afungwe pingu ama kamba.
Taarifa ya polisi Mkoa wa Pwani iliyotolewa kipindi hicho ikielezea tukio hilo ilidai chanzo cha tukio hilo ni magari ya mchanga ya mtuhumiwa, kuharibu barabara na mashamba ya watu yakipita eneo hilo hali iliyosababisha wananchi kufunga barabara kwa magogo kuzuia uharibifu kuendelea.
Katika video hiyo iliyosambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii ambayo ilirekodiwa na Anita Mishu na kuibua mjadala ilionesha Dk Kawambwa, aliyewahi kuwa Mbunge wa Bagamoyo (CCM) akiwa anashambuliwa kwa maneno huku yeye akiwa kimya akishika simu kama vile anafanya mawasiliano.
Leo Jumamosi, Januari 11, 2025, jijini Dar es Salaam, Wembe pamoja na Anita Mushi aliyerekodi tukio hilo wamejitoleza mbele ya waandishi wa habari kuomba radhi huku wakiwa na Dk Kawambwa.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa uamuzi wa Mahakama Kuu kitengo cha Usuluhishi iliyowataka watuhumiwa Wembe na Anita kumwomba radhi Dk Kawambwa ndani ya siku 14 tangu uamuzi huo uliotolewa Desemba 30, 2024.
Wembe ambaye pia mfanyabiashara wa madini amesema wanatambua na kukiri yeye na msaidizi wake (Anita) kwenye biashara walimkosea Dk Kawambwa aliyewahi hudumu wizara mbalimbali ikiwemo ya elimu.
Walikiri kumtendea vitendo vya udhalilishaji na kumtolea maneno ya kashfa, kurekodi na kusambaza video ya tukio hilo kwenye mitandao ya kijamii, wakimtuhumu kwa uongo kuwa Dk Kawambwa ni dalali wa viwanja na mhalifu wa kawaida.”
“Tunaomba radhi kwa Dk Kawambwa, familia yake, wanajimbo la Bagamoyo, jamii na wananchi wote walioona au kusikia tuhuma hizi za uongo. Tunaahidi hatutarudia vitendo kama hivyo tena,” amesema Wembe.
Wembe amesema wanamshukuru Dk Kawambwa kwa moyo wake wa kusamehe na kukubali kumaliza shauri hilo kwa njia ya usuluhishi na kuahidi kushirikiana naye kwenye shughuli mbalimbali akisema ni majirani.
Kwa upande wake, Dk Kawambwa amesema: “Mimi wajibu wangu kama mzee, nimepokea na kukubali kusamehe na limeisha na jambo hili sasa limeisha.”
Alipoulizwa msamaha huo ndio mwelekeo wa kusafishwa na kujiandaa kurudi kwenye ulingo wa siasa, Dk Kawambwa amesema suala hilo lilikuwa Mahakama Kuu Kitengo cha Usuluhisho na lilihitimishwa Desemba 30, 2024 na wahusika kutakiwa kuomba radhi ndani ya siku 14 tangu uamuzi huo.
Amesema ndani ya muda huo wahusika wametekeleza hilo na anawashukuru kwa uungwana wao.