WENYEJI wa michuano ya Kombe la Mapinduzi 2025, Zanzibar Heroes imetinga fainali kwa mbinde na sasa itakutana tena na Burkina Faso iliyowanyoa bao 1-0 katika makundi baada ya juzi usiku kuing’oa Harambee Stars ya Kenya katika mechi iliyojaa matukio yenye utata.
Zanzibar imeifuata Burkina Faso baada ya kumaliza nafasi ya pili ikifikisha pointi sita, ikiiacha Kenya ikiaga ikiwa na alama nne, huku Kilimanjaro Stars ikiondoka Pemba kwa kutofunga bao wala kuvuna pointi yoyote katika mechi tatu ilizocheza.
Burkina Faso iliyotinga mapema fainali baada ya kuizima Kili Stars mabao 2-0 imemaliza vinara kwa kukusanya pointi saba na sasa itavaana na Zanzibar Heroes kesho Jumatatu katika fainali kwenye Uwanja wa Gombani, Pemba itakayotoa bingwa wa michuano ambayo imeshirikisha timu za taifa.
Katika mechi ya Zanzibar kukata tiketi ya kwenda fainali dhidi ya Kenya ilitawaliwa vimbwanga ikiwemo kutolewa kadi mbili nyekundu na nane za njano, huku nahodha wa Harambee Stars Abud Omar alipoonyeshwa kadi nyekundu alikataa kuondoka uwanjani na kuzua vurugu kwa kuishika kadi ile na kutaka kuirarua akimfuata refa kwa nia ya kumpiga.
Hata hivyo, mwamuzi wa pambano hilo alishindwa kuvumilia na kumtuliza kwa kumrushia ngumi ambayo nusra impate Omar ambaye ni miongoni mwa wachezaji wanne wa Harambee waliokuwa wakimzonga refa katika dakika ya 68.
Nahodha huyo alionekana kukerwa mapema baada ya mchezaji mwenzake wa Harambee, Alphonce Omija kuchezewa madhambi nje kidogo ya eneo la hatari na mwamuzi ‘kumeza’ filimbi kabla ya vurugu kutulia na mechi kuendelea kuchezwa huku ikionekana kama ingeisha kwa suluhu.
Kutokana na vurugu zilizosimamisha mchezo na matukio ya kupoteza muda yaliyofanywa zaidi na Wakenya ikiwamo kipa Farouk Shikhalo yalisababisha mchezo kuongezwa dakika 15 zilizosaidia wenyeji kupata bao lililowapeleka fainali likifungwa dakika ya 90+4 kwa kichwa na mtokea benchi Ali Khatib ‘Inzaghi’ aliyemalizia mpira wa kona murua ya Feisal Salum ‘Fei Toto.
Bingwa wa michuano hiyo atavuna Sh100 milioni.