Afrika na mkakati wa kujiondoa gizani

Dar es Salaam. Licha ya juhudi zinazofanywa na mataifa mbalimbali Afrika kuhakikisha upatikanaji wa umeme kwa wananchi wake, zaidi ya nusu ya Waafrika bado hawajafikiwa na huduma hiyo.

Kwa mujibu wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), katika watu wanaokadiriwa kufikia bilioni moja wanaoishi Afrika, takriban milioni 685 hawajafikiwa na huduma ya umeme.

Hali hiyo ya kuwa gizani, inafunga milango ya maendeleo katika baadhi ya mataifa, kwa kuwa umeme ndiyo nyenzo ya kukuza haraka uchumi wa taifa lolote duniani, kama inavyoelezwa na wanazuoni wa uchumi.

Ili kujinasua kutoka katika giza hilo, Wakuu wa Nchi za Afrika wanatarajiwa kukutana Januari 27 na 28, mwaka huu, Dar es Salaam, Tanzania kujadili kuhusu nishati.

Mkutano huo, unaolenga hasa kujadili kuharakisha upatikanaji wa umeme Afrika, pamoja na mambo mengine unalenga kusaka mbinu za kuhakikisha Waafrika milioni 300 wanafikiwa na huduma ya umeme kufikia mwaka 2030 (Ajenda300).

Akizungumzia hilo, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya mkutano huo ambaye pia ni Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Innocent Luoga anasema Benki ya Dunia na AfDB zinalenga kuharakisha upatikanaji wa nishati hiyo kwa Waafrika milioni 300 ifikapo 2030.

Anasema mpango huo, unahusisha nchi zote za Afrika na kwa sasa 14 ndizo zilizochaguliwa kuanza utekelezaji.

Luoga anazitaja nchi hizo ni Tanzania, Mali, Jamhuri ya Demokrasi ya Congo, Ivory Coast, Bukina Faso, Chad, Liberia, Madagascar, Malawi, Mauritania, Msumbiji, Niger, Nigeria na Zambia.

Kwa mujibu wa Kamishna huyo, Tanzania itasaini mpango huo kwa kuwa ni nchi mwenyeji wa mkutano, pia imeshapiga hatua katika usambazaji wa umeme kwa wananchi.

Miongoni mwa yatakayofanyika katika mkutano huo, anasema ni kujadili hali ya upatikanaji wa umeme barani Afrika na kuridhia kwa Azimio la Dar es Salaam la Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu nishati

Pia, anasema kutasainiwa Awamu ya Kwanza ya Mipango Mahsusi ya Kitaifa ya Nishati kwa kipindi cha miaka mitano 2025/30 inayohusisha nchi 14.

“Mkutano huo utafanyika siku mbili. Siku ya kwanza watakutana mawaziri wa nishati na mawaziri wa fedha kutoka nchi za Afrika kwa lengo la kujadili matarajio ya nchi za Afrika kutokana na Ajenda300 na fursa.

“Mageuzi katika sekta ya nishati, upatikanaji wa fedha kwa ajili ya uwekezaji, ushirikishwaji wa sekta binafsi na asasi za kiraia na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia,” anasema.

Luoga anasema kwa sasa Tanzania inaunganishia umeme wateja takriban 500,000 kwa mwaka na katika kipindi cha miaka mitano 2025/30, wateja milioni 2.5 wangeunganishiwa na huduma hiyo.

Lakini, kupitia mpango huo wa Ajenda300, anaeleza Tanzania itakuwa na uwezo wa kuunganishia umeme Watanzania milioni 13.5 yaani karibu mara mbili ya kipindi hicho cha miaka mitano na hivyo kufanya ongezeko la wateja milioni 8.3.

Baada ya kusaini makubaliano ya kuutekeleza mpango huo, Luoga anasema Tanzania inatarajiwa kufikia asilimia 100 ya upatikanaji wa umeme kwa wananchi mwaka 2030.

Anasema inatarajiwa wananchi milioni 13 kufikia mwaka 2030 wataunganishiwa umeme, kasi ya upatikanaji wa nishati safi ya kupikia itaongezeka na umeme wa nishati jadidifu utaongezeka pia.

“Serikali itaishirikisha sekta binafsi katika kutekeleza miradi ya umeme,” anasema.

Akizungumza na Mwananchi kuhusu faida za kiuchumi za mpango huo, Naibu Mkuu wa Chuo, Utawala na Fedha wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Marian, Profesa Benedict Mongula anasema Afrika itabadilika kwa ujumla wake.

Mabadiliko hayo yatatokana na kile alichofafanua, umeme ndiyo nyenzo ya haraka ya kuwezesha uwekezaji kwenye sekta ya viwanda.

“Unapotaka kukuza uchumi wako haraka kama taifa, unahitaji kuwekeza kwenye viwanda, ili uwekeze kwenye viwanda unahitaji umeme. Kwa hiyo mpango huu unakwenda kuinua uchumi wa mataifa ya Afrika,” anasema.

Ukiachana na uwekezaji kwenye viwanda, Profesa Mongula anasema umeme hutumika nyumbani na kuwezesha shughuli mbalimbali zikiwemo za kiuchumi, hivyo utainua kipato cha mtu mmojammoja.

Hata hivyo, anasema Tanzania imepiga hatua katika usambazaji wa umeme na kwamba mpango huo utaongezea kutoka pale ambapo Serikali imeishia.

Hali ya sasa ikoje Tanzania

Mkurugenzi wa Umeme Vijijini wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA), Jones Olotu anasema hadi kufikia Desemba 31, mwaka jana, vijiji vilivyounganishiwa umeme vimefikia 12,301 sawa na asilimia 99.9.

Anasema vijiji 17 vilivyobakia makandarasi wanaendelea na ujenzi wa miundombinu na vinatarajiwa kuunganishiwa itakapofika Januari 31, mwaka huu.

“Tanzania Bara ina jumla ya vitongoji 64,359, vitongoji 33,657 sawa na asilimia 52.3 vimefikiwa na umeme. Vitongoji 30,702 vilivyobaki vipo kwenye mpango wa kupatiwa umeme kwa kipindi cha miaka mitano kulingana na upatikanaji wa fedha,” anasema.

Kwa nini Tanzania mwenyeji

Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Noel Kaganda anasema chimbuko la uenyeji wa Tanzania lilitokana na ombi la Benki ya Dunia na AfDB kwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Anasema Aprili mwaka jana, Benki ya Dunia ilikua na mkutano wa kipupwe Washington, Marekani. Mkutano huo ulikuja na azimio la kuhakikisha Waafrika milioni 300 wanafikiwa na umeme kufikia mwaka 2030.

Baada ya azimio hilo, anasema Rais wa Benki ya Dunia na AfDB waliwasiliana na Rais Samia kumuomba kuwa mwenyekiti wa mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika kuhusu nishati.

Balozi Kaganda anasema Rais Samia aliridhia ombi hilo na ndipo Tanzania ikachaguliwa kuwa mwenyeji.

Akizungumzia kwa nini Tanzania, anasema kwa sababu ni miongoni mwa nchi zinazofanya vizuri katika sekta ya nishati, hadi kufikia Desemba 2024, uzalishaji umeme Tanzania bara ulifikia megawati 3,169.20.

Hali hiyo, anasema umesababisha upatikanaji wa huduma hiyo uongezeke kutoka asilimia 14 mwaka 2011 hadi asilimia 78.4 mwaka 2020.

Sababu nyingine anasema ni Rais Samia amekuwa kinara wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na amefanya hivyo katika majukwaa ya mabadiliko ya tabianchi ya COP 27, 28 na 29, mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika kuhusu nishati safi ya kupikia na mkutano wa G20.

“Tanzania ina mikakati kabambe ya kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika, endelevu na wa gharama nafuu kwa wote hadi kufikia asilimia 75 ifikapo mwaka 2030 na asilimia 80 ifikapo 2034 kwa upande wa nishati safi ya kupikia,” anasema.

Anaitaja sababu nyingine ni kushamiri kwa diplomasia, amani, utulivu, ukarimu na uzoefu.

Related Posts