DC Simanjiro atoa siku 14 wanafunzi wote wawe wameripoti shuleni

Simanjiro. Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Fakii Lulandala ametoa agizo kuhakikisha wanafunzi wote waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza katika shule za sekondari wawe wameanza masomo ifikapo Januari 27, 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumapili Januari 12, 2025 ofisini kwake, Lulandala amesisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi ya wazazi au walezi wa wanafunzi watakaoshindwa kuanza masomo ndani ya muda huo.

Shule za sekondari zinafunguliwa rasmi kesho Jumatatu Januari 13, 2025.

Lulandala amesema wanafunzi 3,248 walihitimu darasa la saba mwaka 2024, wakiwemo wavulana 1,598 na wasichana 1,650. Kati yao, zaidi ya asilimia 98 wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza.

Amesema ufaulu ni mzuri, hivyo wazazi na walezi wawapeleke watoto wao shule wasisubiri kusukumwa kwa kuchukuliwa hatua na Serikali.

“Uboreshaji wa madarasa, nyumba za walimu, vifaa vya kufundishia na upatikanaji wa walimu wa kutosha umefanya mazingira ya shule zetu kuwa rafiki kwa wanafunzi,sioni sababu ya wao kubaki nyumbani” amesema Lulandala.

Amesema kata zote 18 za Wilaya ya Simanjiro zina shule za sekondari na nyingi ziko karibu na makazi ya wananchi, hivyo hakuna kisingizio cha wanafunzi kushindwa kuhudhuria masomo.

Mkazi wa mji mdogo wa Mirerani, Elia Baraka amesema wazazi na walezi wamepunguziwa mzigo wa kuchangia kutoka Sh35,000 hadi Sh20,000.

Kwa upande mwingine, mkazi wa kijiji cha Naberera, Sinyati Mollel ametoa wito kwa Serikali kuwachukulia hatua kali wazazi au walezi wanaowaachisha masomo watoto wao hasa mabinti, kwa kuwaozesha badala ya kuwaendeleza kielimu.

Amesema tabia hiyo inapaswa kudhibitiwa ili kuhakikisha watoto wote wanapata haki yao ya msingi ya elimu.

Related Posts