Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, jana aliongoza wananchi na viongozi mbalimbali katika kuadhimisha miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar katika sherehe zilizofanyika Gombani, Chake Chake, Pemba.
Makomando wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ni miongoni mwa waliokuwa kivutio kikubwa katika kilele cha maadhimisho hayo ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Miongoni mwa viongozi waliohudhuria sherehe hizo ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, makamu wake, Dk Philip Mpango, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko, na Makamu wa Kwanza na wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud na Hemed Suleiman Abdulla.
Aidha, marais wastaafu wa Tanzania na Zanzibar, mawaziri, na viongozi wengine wa serikali walikuwepo.
Katika onyesho la kwanza, makomandoo wawili walipita mbele ya Rais Mwinyi na viongozi wengine wakiwa wamebeba mbwa wawili wa kivita mgongoni. Kitendo hicho kilionyesha mbinu za kukabiliana na changamoto za kivita, hususan wanapokutana na mazingira magumu kama maji au maeneo ambapo mbwa hawawezi kupita kwa urahisi. Hali hii ililenga kuhakikisha usalama wa mbwa hao dhidi ya hatari zinazoweza kujitokeza.
Katika onyesho lingine la kivita, wanajeshi wakiwa na mbwa walifanikiwa kumkamata muasi aliyekuwa akijaribu kutoroka porini. Helikopta ya kijeshi ilifika ikiwa na wanajeshi na mbwa mmoja wa kivita. Wanajeshi waliposhuka kutoka kwenye helikopta hiyo, mbwa huyo alielekezwa kumdhibiti muasi mpaka aliposalimishwa mikononi mwa askari.
Baada ya muasi kukamatwa, helikopta hiyo ilirudi karibu na ardhi na kutumia kamba maalumu kuwavuta wanajeshi pamoja na muasi aliyekamatwa, kisha wakaondoka naye.
Wakati maonyesho hayo yakifanyika, wananchi na viongozi waliokuwa uwanjani walionyesha shauku kubwa kwa kushangilia na kufuatilia kwa makini kila tukio.
Kabla ya maonyesho haya, Dk Mwinyi aliingia uwanjani akiwa ndani ya gari maalumu la wazi, likiongozwa na pikipiki tano. Aliwapungia mkono wananchi, huku akilakiwa kwa shangwe, vifijo na nderemo.
Baadaye, alipokea salamu ya Rais, kupigiwa mizinga 21, na kushuhudia maandamano ya wananchi yaliyoshirikisha wawakilishi kutoka mikoa mbalimbali ya Unguja na Pemba.
Maandamano hayo yalihusisha wananchi kutoka mikoa yote ya Unguja na Pemba, wakiwa na mabango yenye ujumbe wa kuadhimisha miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Kipengele kilichovutia zaidi katika gwaride lililoshirikisha wanajeshi, polisi, magereza, zimamoto, na vikosi vya SMZ ni pale walipounda umbo la namba 61, likiwa ni ishara ya kumbukumbu ya miaka ya Mapinduzi.
Akitoa shukrani na salamu kwa wananchi na viongozi waliohudhuria sherehe hizo, Rais Mwinyi alisema Serikali imetafsiri dhamira ya Mapinduzi kwa kuleta mageuzi makubwa ya kiuchumi, kisiasa, na kijamii, hatua iliyochangia kukuza uchumi kupitia ongezeko la mapato na udhibiti mzuri wa matumizi.
Alisisitiza kuwa siku hiyo ni muhimu kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, kwani inaadhimisha miaka 61 tangu wazee waasisi walipojitoa mhanga na kufanya Mapinduzi, siku ambayo ilifungua ukurasa mpya wa ukombozi wa kiuchumi, kisiasa, na kijamii dhidi ya madhila ya utawala wa kikoloni.
“Natoa pongezi kwa wananchi kwa mafanikio tuliyopata katika miaka 61 ya Mapinduzi. Ni wajibu wetu kuendeleza amani, mshikamano, na maendeleo kwa manufaa ya taifa,” alisema Dk Mwinyi.
Katika hotuba yake ya takribani dakika 10, aliongeza kuwa mafanikio yaliyofikiwa yameleta umoja na usawa kwa wananchi wote kunufaika na rasilimali na fursa kwa usawa.
Pia alihimiza wananchi kuendeleza bidii, uadilifu, uaminifu, na uzalendo kwa kuweka mbele maslahi ya taifa kama ilivyokuwa nia ya waasisi wa Mapinduzi.
Kuhusu uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, Dk Mwinyi alihimiza wananchi kushiriki kwa amani na kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa utulivu kabla, wakati, na baada ya zoezi hilo.
Alibainisha kuwa tume za uchaguzi tayari zimeanza maandalizi kwa kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa haki na kufuata sheria, na akasisitiza ushirikiano wa wananchi na tume hizo.
Awali, Makamu wa Pili wa Rais, Hemed Suleiman Abdulla, alisifu juhudi za viongozi wa kitaifa, akiwemo Rais Samia na Dk Mwinyi, katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo.
Hemed, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Sherehe za Kitaifa, alisema shamrashamra za Mapinduzi zilianza rasmi Desemba 15, 2024, zikijumuisha uzinduzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo katika visiwa vya Unguja na Pemba.
“Miradi yote tuliyofungua na kuzindua imeleta hamasa kubwa. Hii ni ishara ya mshikamano wa wananchi wetu. Hivyo, tuendelee kudumisha umoja huo na kupiga hatua zaidi za maendeleo,” alisema Hemed.