Hii hapa ratiba nzima sherehe ya Mapinduzi Zanzibar

Unguja. Leo ikiwa ni kilele cha maadhimisho ya miaka 61 ya Mapinduzi ya Zanzibar, wananchi wameanza kuingia katika Uwanja wa Gombani, Wilaya ya Chakechake, Mkoa wa Kusini Pemba zinapofanyika sherehe hizo.

Katika sherehe hizo ambazo wageni waalikwa na viongozi mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kuanza kuingia uwanjani hapo kuanzia saa 6:35 mchana, zitaongozwa na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi huku akitarajiwa kutoa neno la shukrani na kuwasalimia wananchi kati ya saa 9:55 hadi saa 10:05 jioni.

Wageni wengine watakaohudhuria sherehe hizo leo Januari 12, 2025 ni Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais,  Dk Philip Mpango, Makamu wa Rais wa kwanza na wa Pili wa Zanzibar, Waziri Mkuu, Naibu Waziri Mkuu marais wastaafu na viongozi wakuu wa Tanzania Bara na Visiwani.

Milango ya uwanja huo imefunguliwa kuanzia saa 4:00 asubuhi na kwa mujibu wa ratiba ya sherehe hizo ambazo mwenyekiti wake ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla, wageni waalikwa wataanza kuingia katika uwanja huo saa 6:30 mchana.

Mabalozi na viongozi wa mashirika ya kimataifa pamoja na mawaziri wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania watawasili uwanjani saa 6:35 hadi saa6:45 mchana.

Viongozi wakuu wastaafu wataingia kati ya saa 6:45 hadi saa 6:55 mchana wakifuatiwa na majaji wakuu; Profesa Ibrahim Juma (Tanzania bara) na Jaji Khamis Ramadhan Abdalla (Zanzibar) saa 7:00 mchana.

Viongozi wengine watakaoingia uwanjani hapo ni Spika wa Tanzania, Dk Tulia Ackson na yule wa Zanzibar, Zubeir Maulid watawasili saa 7:05 mchana wakifuatiwa na marais wastaafu Aman Abeid Karume, Dk Ali Mohemd Shein na Jakaya Kikwete.

Kati ya saa 7:10 hadi saa 7:20 mchana wataingia, Mkuu wa majeshi ya Ulinzi, Jenerali Jacob Nkunda, Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko kisha kufuatiwa na Makamu wa Pili wa Rais na wa kwanza, Hemed Suleiman Abdula na Othman Masoud.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa atawasili uwanjani hapa saa 7:35 akifuatiwa na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango saa 7:45 mchana wakifuatiwa na viongozi wakuu wa nchi mbalimbali waalikwa na kisha gwaride kuingia uwanjani.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, Rais Samia Suluhu Hassan atawasili uwanjani hapo saa 8:05 mchana na kupokea salamu, akifuatiwa na Rais wa Zanzibar atakayeingia uwanjani saa 8:25 naye atapokea salamu ya Rais na mizinga 21 itapigwa.

Baada ya kuingia, kati ya saa 8:25 hadi saa 8:40 mchana Dk Mwinyi atapokea maandamano ya wananchi kisha gwaride litasonga mbele yake na kutoa salamu ya utii kisha kuimbwa wimbo wa Taifa wa Zanzibar na wimbo maalumu wa mashujaa kisha kufanya maonyesho maalumu.

Kwa mujibu wa ratiba, kati ya saa 9:55 -hadi saa 10:05 jioni, Rais Mwinyi atatoa neno la shukrani na kuwasalimia viongozi, wageni waalikwa na wananchi.

Related Posts