Januari, mwezi unaojulikana kama “Januari ngumu,” ni kipindi ambacho familia nyingi hupitia changamoto za kifedha baada ya matumizi makubwa wakati wa msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka.
Hata hivyo, kwa baadhi ya watu, changamoto hizi zimekuwa historia, shukrani kwa vikundi vya kuweka na kukopa, maarufu kama vikoba, ambavyo vimekuwa msaada muhimu wakati wa matatizo ya kifedha kwa baadhi ya familia ambazo zina wanachama wake.
Wanachama hao, ambao ni pamoja na mama na baba kwenye familia, wengi wao wanakiri kuwa kupitia akiba na mikopo inayotolewa katika vikundi hivyo, wameweza kulipa ada za shule kwa watoto, kodi za nyumba na hata kuanzisha biashara ndogondogo. Ingawa bado kuna baadhi ya wanaume wanashawishika taratibu kujiunga na vikoba, wapo waliowaunga mkono wenza wao na kushuhudia manufaa yake, hasa wanapokabiliana na changamoto za kifedha.
Januari ni kipindi kinachofahamika kwa wengi kama wakati mgumu wa kifedha, ambapo watu wengi wanakabiliwa na mahitaji mbalimbali ya fedha. Baadhi hulazimika kulipa kodi, ada za shule za watoto, kununua vifaa vya shule kama sare na madaftari, na mahitaji mengine muhimu
Hata hivyo, wale waliojiunga na vikoba wameweza kukabiliana na changamoto hizi kwa urahisi zaidi. Wapo wanaosema kuwa vimewasaidia kuvuna kile walichowekeza kwa mwaka mzima au hata kwa kipindi cha miaka miwili.
Mgawo wa fedha za vikoba mara nyingine hufanyika ndani ya Oktoba mpaka Februari, miezi yenye uhitaji mkubwa wa fedha kwa familia nyingi.
Kwa sababu fedha hizo huweza kutumika katika kutekeleza majukumu msingi ya familia bila wasiwasi wowote.
Na baadhi ya wanachama wa vikoba ndiyo muda ambao hujipongeza kwa kufanikisha malengo yao ya kifedha kwa kuandaa sherehe au safari, ndani na nje ya nchi, kama njia ya kusherehekea mafanikio yao.
Kutokana na hilo, Mwananchi imezungumza na baadhi ya washiriki wa vikundi vya vikoba na kuelezea namna vinavyoweza kuikomboa familia pale inapopitia kwenye wakati mgumu wa uhitaji wa fedha.
Akizungumza na Mwananchi, mkazi wa Mbagala, jijini Dar es Salaam, Fatma Hamis anasema wakati wengine wakihangaika na Januari hii, kwake kuko slama kama si mwanzo wa mwaka.
“Kikoba chetu tumekivunja Desemba, na Januari hii niliweka malengo kadhaa kuhusu watoto wangu, yametimia, nimejikuta ninautua mzigo mapema sana, nilishalipa ada za watoto wetu kabla ya sikukuu na hapa nilipo sidaiwi,” anasema Fatma.
Anasema asilimia kubwa ya wanachama wa vikoba ni wanawake, hata walioolewa ambao wanatoa shuhuda kadhaa za namna vikoba vinavyoneemesha familia zao.
“Lakini pia kupitia vikoba, wanawake wengi wamepata maendeleo ya mitaji na sasa wanajimudu, si tegemezi tena, hata waume zao wanawasifu kwa kusaidia familia zao,” anasema Hamis.
Anatolea mfano kipindi hiki ambacho shule zinafunguliwa: “Kwenye kikundi chetu ambacho tupo wanawake watupu, baadhi wanatuambia fedha za vikoba tukivunja huwa wanasaidiana na waume zao kulipa ada za shule za watoto na kununua mahitaji mengine muhimu.”
Hata hivyo, anasema ili mtu aweze kuona faida ya fedha hizo, ni kuwa na nidhamu tu ya matumizi ya fedha hizo.
“Mfano mimi awali nilikuwa limbukeni wa hizi hela, tulikuwa tukivunja mwezi wa 12, nazitumia hovyo kwenye sikukuu halafu ikifika mwezi kama huu (Januari) watoto wanafungua shule nakuwa sina hata mia, narudi kukopa kila kona, faida nakuwa siioni, lakini nimejifunza, sasa hivi niko sawa kabisa,” anasema Hamisi.
Anasema alikuwa mkopaji mzuri wa mikopo ya mitaani mpaka ilifikia hatua akawa anashindwa kuelewana na mumewe na hata ndugu zake pia kwa sababu ya madeni.
Hata hivyo, anasema tatizo hilo lilitibika baada ya kukalishwa chini na baadhi ya watu waliomshawishi ajiunge na kikundi cha kikoba na akapatiwa elimu ya fedha, sasa anaona matunda yake.
“Januari siku hizi kwangu ni mteremko kwa sababu kikoba chetu huwa tunavunja Desemba katikati, hivyo mimi na familia yangu huwa tunapanga namna nzuri ya kuzitumia fedha hizi,” anasema.
Naye, dereva wa bodaboda kutoka Kigamboni, Hassan Salum anasema vikoba vimeleta mabadiliko makubwa kwenye maisha yake.
“Nilijiunga na kikoba wanaume tukiwa watano tu, na tulikubaliana kila mmoja ajiwekee malengo kwa ajili ya Januari, namshukuru Mungu kila jambo tumelifanikisha, kilio cha watu wengi mwanzoni mwa mwaka, kwa familia yangu ni kicheko, safari hii nimevuna Sh2 milioni na tumetimiza malengo yetu,” anasema Hassan.
Anasema amekuwa na tabia ya kutotoa michango ya sherehe inapofika Desemba kwa sababu ya kuwekeza pesa zake na kupambana na Januari ambayo imepitiwa na sikukuu na wageni wengi nyumbani kwake.
“Na uzuri wa hizi hela, tunatumiwa moja kwa moja kwenye akaunti ya benki, kwa hiyo siyo rahisi kuzitumia ovyo ovyo tofauti na malengo niliyojiwekea ya maendeleo kwa ajili ya familia yangu,” anasema.
Anasema awali alikuwa akigombana na mkewe kuhusu matumizi mabaya ya fedha, lakini tangu ajiunge na kikoba ambako pia hupatiwa elimu ya miradi na fedha, ile hali ameiacha.
Hivyo, Salum anasema kikoba kimekuwa chanzo cha kupanga bajeti ya familia na mkewe kulingana na kipato wanachokiingiza.
“Kutokana na kipato kinachopatikana wameweza kujadili na kujenga na kwa sasa hawalipi tena kodi zaidi ya ada za watoto ambapo awali walikuwa wanasoma shule za kawaida, lakini sasa kawapeleka katika shule za kulipia.
“Nilikuwa sielewi nilivyokuwa naona baadhi ya watu kijiweni hawalalamiki kuhusu ugumu wa Januari, katika mazungmzo husikii wakigusia jambo hilo hadi najiuliza au kuna mahali nakosea, ndipo nilipotonywa kuwa mpango mzima ni vikoba,” anasema Salum.
Wanawake wanaoshiriki katika vikoba wanasema wanapanga bajeti zao mapema kwa kutumia mikopo wanayochukua au akiba wanayoweka kupitia vikundi hivi.
“Nilijifunza kuweka akiba kidogo kidogo kila mwezi kupitia kikoba changu, na sasa Januari si changamoto tena kwangu,” anasema Veronica Vicent, mama wa watoto watatu kutoka Kinondoni, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Veronica, akiba anayopata kupitia kikoba imemwezesha kulipia ada za watoto wake bila kutegemea msaada wa dharura. Hali hii imesaidia kupunguza mzigo kwa wanafamilia wengine, hususan waume zao, ambao mara nyingi hubeba gharama zote.
Mtaalamu wa masuala ya uchumi, Jane Prosper, anasema vikoba vinaweza kuwa suluhisho bora kwa changamoto za kifedha endapo washiriki watajifunza kupanga matumizi kwa ufanisi.
“Wanawake wanapojifunza kuweka akiba kidogo kidogo, wanapata uwezo wa kushughulikia changamoto kubwa za kifedha kama ada za shule bila kuingia kwenye madeni yasiyo ya lazima,” anasema Jane.
Hata hivyo, Jane ameonya juu ya matumizi mabaya ya mikopo ya vikoba, kama vile kuelekeza fedha kwenye sherehe badala ya maendeleo ya familia. Amehimiza umuhimu wa mafunzo ya usimamizi wa fedha kwa wanachama wa vikoba ili kuhakikisha fedha zinatumika kwa manufaa.
Kwa upande wake, Ofisa Ustawi wa Jamii wa Jijini Mbeya, Mary Marcus, anaeleza kuwa vikoba vina mchango mkubwa si tu kwa maendeleo ya kiuchumi, bali pia kwa ustawi wa familia.
“Wanawake wanaposhiriki katika kugharimia mahitaji ya familia kama kulipa ada na kodi, wanawapunguzia waume zao mzigo wa kifedha na kuongeza mshikamano wa kifamilia,” anasema Mary.
Aidha, Mary anabainisha kuwa wanawake wanaoshiriki vikoba wamepata uwezo wa kutatua changamoto za kifamilia, jambo lililopunguza migogoro ya kifamilia.
“Zamani tulikuwa tunapokea kesi nyingi za watu kususia familia na kukimbia majukumu. Siku hizi, hali imebadilika kwa kiasi kikubwa, na hata baadhi ya wanaume sasa huja kutaka ushauri juu ya majukumu yao kama vichwa vya familia kwa sababu hawapigiwi kelele kuhusu matumizi ya nyumbani,” anasema.