JKT Queens kama ilivyo kawaida yake ya kusajili wachezaji chipukuzi ambao wanafanya vizuri, tayari imenasa saini za wachezaji wapya wawili makinda wenye vipaji.
Wachezaji hao ni beki wa kati, Aneth Masala kutoka Allan Queens ya Dodoma na kiungo mshambuliaji, Elizabeth John kutoka Alliance Girls.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na uongozi wa Allan Queens, Masala sasa ni mali halali ya JKT baada ya kukamilisha taratibu zote za uhamisho katika dirisha hili dogo la usajili.
“Kapteni wetu amejiunga na JKT kwa makubaliano ya pande zote tatu, tunaushukuru uongozi wa JKT kwa kushirikiana nasi hadi kukamilisha taratibu zote.”
Beki huyo tayari ameanza kuvaa uzi wa JKT tangu wiki iliyopita kwenye mashindano ya vijana.
Vivyo hivyo kwa Alliance ilithibitisha kiungo huyo kujiunga na wanajeshi hao wa kike kwa makubaliano ambayo hayakuwekwa wazi.
Elizabeth alikuwa na kiwango bora kwenye Ligi tangu msimu uliopita na msimu huu amekuwa na muendelezo uliowavutia mabosi wa JKT.
Mwanaspoti ilipomtafuta Katibu Mkuu wa JKT Queens, Duncan Maliyabwana kuthibitisha uhamisho wa mchezaji huyo anayetarajiwa kufanya makubwa, hakupatikana.