Januari 12, 1964, visiwa vya Zanzibar vilijikuta katika hali ya mabadiliko yaliyotokana na mgongano wa itikadi, historia na matarajio ya wengi.
Chini ya utawala wa Sultani, uliokuwa ukiegemea chama cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP), wananchi wengi wenye asili ya Afrika walijikuta wakikumbana na ukandamizaji wa kisiasa na kijamii. Haki za msingi ziliporwa, huku walio wengi wakinyimwa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika uamuzi wa mustakabali wa nchi yao.
Uchaguzi uliojaa ubaguzi na mizengwe ulizidisha hali ya taharuki, ukiacha maswali mengi yasiyo na majibu miongoni mwa wananchi waliokuwa wakitamani mabadiliko.
Wanahistoria na wasomi mbalimbali wanaweka wazi kilichochochea kufanyika kwa mapinduzi hayo, huku ukandamizaji, unyonywaji wa Waafrika walio wengi zikiwa ni miongoni mwa sababu. Hayo yanakuja ikiwa imepita miaka 61 tangu mapinduzi hayo yalipofanyika na Sheikh Abeid Amani Karume akawa Rais wa kwanza wa Zanzibar.
Mbunge wa Afrika Mashariki, Abdulla Hasnu Makame anasema umuhimu wa uamuzi wa kufanyika kwa mapinduzi mwaka 1964, ulitokana na kuwepo kwa hali ya ubaguzi dhidi ya watu wenye asili ya Afrika.
Makame anasema ubaguzi huo ulifanyika kupitia chama cha Zanzibar Nationalist Party (ZNP) kilichoongoza Serikali kwa wakati huo.
“Katika sera zake za kibaguzi, kuna wakati walikataa kushiriki katika vikao halali vya kupinga sheria kwa sababu eti hawawezi kukaa meza moja na watu ambao si wastaarabu, yaani watu weusi, hii ilitokea mwaka 1957,” anasema.
Anaeleza kuwa baadaye mmoja wa wafuasi wa chama hicho, aliyefahamika kwa jina la Al-Mukheir, alisema hatakubali kuona ubaguzi huo unafanyika na akawa anaenda kwenye vikao.
Kwa sababu ya alichokifanya Al-Mukheir, Makame anaeleza kuwa mtu mmoja kutoka katika chama hicho alimchoma kisu na alipolazwa hospitali, alikwenda kummalizia, akapoteza maisha.
“Huu ni mfano tu kwamba kulikuwa na mfumo wa kibaguzi dhidi ya Waafrika walio wengi na kwa bahati nzuri, kiongozi wa wakati huo, ambaye alikuwa Sultani na kwa nafasi yake hakutakiwa kuegemea upande wowote, yeye aliegemea kwa ZNP,” anasema.
Mazingira hayo, anasema yalilazimu mapinduzi yafanyike na dhamira yake hasa ilikuwa ni kupingana na kuondokana na ubaguzi wa rangi.
Akizungumzia hilo, mtoto wa pili wa Sheikh Abeid Amani Karume, Balozi Ali Karume anasema ubadhirifu katika uchaguzi ndiyo uliochochea mapinduzi.
Kwa mujibu wa Balozi Karume, Uingereza ilitoa sharti ili litoe uhuru unapaswa kufanyika uchaguzi na chama kitakachoshinda ndicho kitakachopewa nchi.
Kabla ya kufanyika uchaguzi, anasema ililazimika kwanza viundwe vyama vya siasa na yalipotekelezwa hayo, ulianza kufanywa uchaguzi mdogo.
Kwa mtazamo wa Balozi Karume, uchaguzi mdogo uliofanywa mwaka 1957 ulilenga kupima uwezo wa vyama vilivyokuwepo kujua iwapo vinaweza kushinda na kukabidhiwa uhuru au vinginevyo.
Katika uchaguzi huo, anaeleza kulikuwa na viti sita na vitano miongoni mwa hivyo kilishinda chama cha ASP na kimoja alishinda mgombea binafsi aliyekuwa Mhindi.
Baadaye mwaka 1959, anasema kiliundwa chama kingine cha siasa cha ZPPP na wakati huo, Uingereza waliweka wazi kuwa utawala utakuwa wa kisultani, hivyo uchaguzi utafanywa kwa nafasi za ubunge pekee.
Januari mwaka 1961, anasema ukafanyika uchaguzi na viti viliongezwa, hivyo matokeo yakawa ASP ilipata viti 10, ZNP sita, ZPPP vitatu.
Pamoja na ASP kupata viti vingi, anasema hakikupewa nafasi ya kuunda Serikali, hivyo kulikuwa na vurugu na walipelekwa askari kutoka Kenya na Scotland kutuliza hali iliyokuwepo.
“Wakakubaliana kufanyika kwa uchaguzi mwingine mwaka 1963 na kabla Waingereza walisema pengine iundwe Serikali ya muungano,” anasema.
Anasema kukatokea mgawanyiko katika vyama, baadhi ya wanasiasa kutoka ZNP na ZPPP walihamia ASP na kikakosekana chama ambacho kingeunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
Mwaka 1963, anasema uchaguzi ukafanyika na ASP ilishinda viti 13, ZNP 12, ZPPP sita na yakafanyika mazingira ASP haikupewa nchi kwa mara nyingine.
Hata waziri mkuu hakutokana na ASP, badala yake wadhifa huo ulishikwa na mtu kutoka chama cha ZPPP.
Hali hiyo, ilizusha hasira kwa wananchi na haja ya mapinduzi ilizidi na hatimaye yakafanyika Unguja.
“Kwa bahati, mzee wangu Karume (Sheikh Abeid) alikuwa anatunza siri, sikuwahi kumsikia akitamka na niliwahi kumsikia Mzee Jumbe (Aboud) akitamka hatutasubiri uchaguzi, tutawachapa bakora,” anasema.
Kwa mtazamo wa mwanahistoria, Profesa Abdul Sheriff, Mapinduzi ya Zanzibar yalifanyika yakilenga kuunganisha wananchi, lakini matokeo yakawa vinginevyo.
Anaeleza kuwa licha ya dhamira ya mapinduzi hayo kutengeneza Taifa lenye umoja, bado kuna mgawanyiko wa watu katika visiwa hivyo.
Kwa mujibu wa mwanazuoni huyo, enzi hizo kulikuwepo na vyama vya kikabila na ukabila ulishika kasi, katika eneo ambalo waliishi watu kutoka mataifa mbalimbali.
Baada ya mwingiliano wa watu kutoka maeneo mbalimbali na wote wanazungumza Kiswahili, anasema kukaanza kuibuka juhudi za kutafuta muungano wa watu wawe wamoja kama nchi.
“Wakasema tukishindana kikabila tutauana, vikaanza kuundwa vyama vya kitaifa ZNP na vingine, huku Pemba wakitaka iendelee kama ilivyo ili inufaike na rasilimali ilizonazo na zile inazozalisha,” anaeleza.
Baada ya uchaguzi ambao ungeamua kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, anasema mambo yalivurugika na ndipo vuguvugu la muungano lilipoanza.
Kwa mujibu wa Profesa Sherrif, ASP walikataa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa baada ya kushawishiwa na kuahidiwa kwamba yatafanyika mambo.
Pamoja na yote hayo kufanyika, anasema bado hadi sasa visiwa hivyo vimegawanyika.
“Hadi sasa nchi imegawanyika nusu kwa nusu, wapo watu kutoka mataifa mbalimbali waliokaa hapa Zanzibar kwa miaka 200 hadi 300 hawana kwingine kwa kwenda, lakini bado hawaitwi Wazanzibari.
“Mimi nimezaliwa Zanzibar lakini babu yangu alikuja Zanzibar na alijenga nyumba miaka iliyopita, hivi leo utaniita mimi Mhindi au Mzanzibari?” anahoji.