Maria Sarungi adaiwa kutekwa Nairobi

Dar es Salaam. Mwanaharakati, Maria Sarungi ambaye kwa sasa anaishi nchini Kenya ameripotiwa kutekwa na watu wasiojulikana leo nchini humo.

Taarifa iliyochapishwa katika ukurasa wa Instagram wa Daily Nation, leo Jumapili Januari 12, 2025 imeeleza: “Maria Sarungi Tsehai, mhariri huru wa vyombo vya habari nchini Tanzania na mtetezi wa haki za binadamu, ametekwa nyara na watu watatu wenye silaha katika eneo la Chaka, Kilimani jijini Nairobi, kwa mujibu wa Amnesty International-Kenya.”

Juhudi za kuwapata Polisi nchini Kenya kuzungumzia tukio hilo zinaendelea.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)-Bara, Tundu Lissu ameitaka Serikali ya Kenya kuingilia kati madai hayo ya kutekwa kwa mwanaharakati huyo.

Mbali ya Daily Nation, taarifa za kutekwa kwa Maria zimesambaa leo Jumapili Januari 12, 2025 baada ya mtandao wa kimataifa wa haki za binadamu wa Amnesty International kuripoti taarifa hiyo.

“Maria alikuwa amekimbilia uhamishoni nchini Kenya tangu kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 ambapo amekuwa akiendesha televisheni ya mtandaoni ya Mwanzo TV, inayotoa maudhui ya kuunga mkono demokrasia.

“Ingawa tunatumaini na kusali kwa ajili ya maisha na usalama wa Maria, ni lazima tutoe wito kwa Serikali ya Kenya na watu wote wenye nia njema kutoka duniani kote kuingilia kati, kuhakikisha usalama wa Maria,”ameandika Lissu.

Kwa sasa nchi ya Kenya inagubikwa na matukio mengi ya utekaji, jambo lililosababisha mgomo wa wananchi wiki iliyopita kushinikiza kupatikana kwa watu waliotoweka.

Tovuti ya Daily Nation Januari 6, 2025 iliripoti kuwa vijana wanne kati ya 29 walioripotiwa kutekwa na watu wasiojulikana nchini Kenya, walipatikana wakiwa hai huku familia zao zikithibitisha.

Vijana hao wanaotajwa kuwa wakosoaji wa Serikali ya awamu ya tano ya nchi hiyo, walianza kutoweka mwishoni mwa mwaka 2024, jambo lililosababisha baadhi ya Wakenya kuandaa maandamano kuitaka Serikali iwarudishe.

Vijana hao waliopatikana Jumatatu, Januari 6, 2025 ni pamoja na Billy Munyiri Mwangi (24), Peter Muteti (22), Bernard Kavuli na Ronny Kiplagat.

Hii sio mara ya kwanza kwa mwanaharakati wa nchi nyingine kudaiwa kutekwa Kenya,  Novemba 16, 2024, Kiongozi wa chama cha upinzani cha Uganda, Forum for Democratic Change (FDC), Dk Kizza Besigye alitekwa jijini Nairobi na kupelekwa Uganda, ambako alisomewa mashtaka mbalimbali katika mahakama ya kijeshi na kesi yake bado inaendelea.

Related Posts