Mbegu atimkia Mashujaa FC | Mwanaspoti

BEKI wa kushoto wa Singida Black Stars, Yahya Mbegu ametolewa kwa mkopo kwenda kuitumikia timu ya maafande wa Mashujaa FC ya mkoani Kigoma hadi mwisho wa msimu huu, baada ya nyota huyo kushindwa kupenya kikosi cha kwanza mara kwa mara.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari na Mawasiliano wa Singida Black Stars, Hussein Massanza alikiri Mbegu kutolewa kwa mkopo wa miezi sita kwenda Mashujaa, huku akiweka wazi wameangalia namna nzuri ya kumpeleka timu atakayocheza zaidi.

“Wachezaji wote tunaowatoa kwa mikopo haina maana sio wazuri isipokuwa ni suala la ushindani tu na tunachohitaji sisi ni kuona wanapata nafasi ya kucheza mara kwa mara ili kulinda vipaji vyao, matumaini yetu kwao ni makubwa huko mbele.”

Mwenyekiti wa Mashujaa, Meja Abdul Tika alisema licha ya kikosi hicho kuonekana kusuasua katika usajili, mashabiki wao watarajie mambo mazuri, kwani wao kama viongozi wanafanya kila kinachowezekana kupata saini ya nyota walio bora.

Mbegu aliyewahi kucheza timu mbalimbali zikiwamo za Geita Gold na Polisi Tanzania, ameshindwa kupenya kikosi cha kwanza cha Singida kutokana na uwepo wa beki raia wa Ghana, Ibrahim Imoro aliyejiunga na timu hiyo akitokea Al Hilal ya Sudan.

Usajili huo wa Mbegu ni wa kwanza ndani ya kikosi hicho cha Mashujaa katika dirisha hili dogo, japo taarifa zilizopo zinadai viongozi wa timu hiyo wanaiwinda saini ya mshambuliaji, Danny Lyanga wa JKT Tanzania.

Related Posts