MKURUGENZI WA TIBA MUHIMBILI ATEULIWA KUWA MKUU WA KITENGO CHA HUDUMA ZA TIBA UMOJA WA AFRIKA (AU)

Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dkt. John Rwegasha ameteuliwa kushika wadhifa wa Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Tiba, Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) yenye makao makuu yake nchini Addis Ababa, Ethiopia ambapo anatarajiwa kuanza kazi Februari, 2025.

Akiagana na Menejimenti ya MNH mwishoni mwa wiki hii, Dkt. Rwegasha amesema anamshukuru Mungu kwa nafasi hiyo ambayo ilikua na ushindani mkubwa katika mchakato wa usaili na yeye kufanikiwa kufaulu na hatimaye kuteuliwa rasmi kati ya washindani wenzake kutoka mataifa saba ya Afrika.

Akitoa salamu za pongezi, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Prof. Mohamed Janabi ambaye pia ni Mshauri wa Rais Masuala ya Afya na Tiba amemtakia kila la kheri na uwakilishi mzuri wa Tanzania katika kutekeleza majukumu yake katika chombo kikubwa cha Umoja wa Afrika hususani katika eneo la sekta ya afya barani Afrika.

Dkt. Rwegasha ni Daktari Bingwa Mbobezi wa Magonjwa ya Mfumo wa Chakula na Ini ambaye kutokana na jitihada zake alifanikisha MNH kuanzisha kituo cha utoaji mafunzo na tiba ya ugonjwa huo nchini mwaka 2013 na kuwa Mkuu wa Kitengo hicho hadi mwaka 2018 alipoteuliwa kuwa Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Ndani yenye Vitengo 11 na badaye Oktoba 2022 aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Huduma za Tiba MNH ambapo alikua akisimamia idara saba.

Kuhusu elimu, Dkt. Rwegasha ana Shahada ya Kwanza ya Udaktari ya Chuo Kikuu cha Makerere, Shahada ya Uzamili ya Udaktari ya Chuo Kikuu cha Aga Khan Kenya, Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Uongozi ya Chuo Kikuu Mzumbe, Stashahada ya Usimamizi wa Afya ya Chuo Kikuu cha Washington nchini Marekani pamoja na utambulisho mwingine kadhaa wa kitaaluma katika tiba kutoka vyuo vikuu nchini Uingereza na Afrika ya Kusini.


 

Related Posts