Mmiliki Afunguka Kwa nini Nyumba Yake Haikuungua – Global Publishers

Siku chache zilizopita, habari kuhusu nyumba pekee iliyonusurika na moto katika Ufukwe wa Malibu, Los Angeles nchini Marekani, ilizua gumzo duniani kote, kila mtu akiongea lake.

Mmiliki wa nyumba hiyo yenye thamani ya dola milioni 9 za Kimarekani (sawa na takribani shilingi bilioni 22.5 za Kibongo), David Steiner ameeleza sababu za nyumba yake kusalimika.

Bilionea huyo anayeishi Texas, akiwa ni baba wa watoto watatu, amesema wakati anaijenga nyumba hiyo, alizingatia uimara na ubora wa kila kitu akitaka iwe na uwezo wa kuhimili matetemeko yanayotokea mara kwa mara.

“Ilibuniwa kustahimili matetemeko ya ardhi na ina ujenzi imara sana. Kuta zake ni za mawe, zege na saruji na paa lake lilitengenezwa kwa mfumo wa kuzuia lisishike moto.

David Steiner

“Nguzo za msingi pia zilichimbiwa futi 50 kwenda chini ili kuhimili hata mawimbi makali ya maji ya bahari,” alisema na kuongeza kuwa alitaka iwe sehemu salama ya kukimbilia iwapo kutatokea tetemeko.

“Kiukweli sikufikiria kabisa kwamba hata baada ya miaka milioni moja, moto unaweza kuja kusababisha uharibifu kwenye ufukwe wa Bahari ya Pacific,” Steiner aliliambia Gazeti la The New York Post.

Akielezea jinsi alivyopata taarifa, Steiner amesema yeye na familia yake hawaishi ndani ya nyumba hiyo na kwamba siku ya tukio, alikuwa nyumbani kwake, Texas.

Fundi mmoja aliyekuwa akifuatilia habari za moto kwenye runinga, alimtumia video ikionesha nyumba zote zilizopo jirani na nyumba yake zinawaka moto na akamwambia anahisi na yake pia itaungua.

Steiner anaeleza kuwa alipoiona video hiyo, hata yeye mwenyewe alikata tamaa akiamini nyumba yake itateketea lakini saa chache baadaye, anaeleza kuwa alianza kupigiwa simu nyingi na watu waliokuwa wanamueleza kuwa nyumba yake inaoneshwa kwenye vyombo vya habari.

Anasema alipofuatilia, ndipo alipogundua kwamba kumbe nyumba yake ilikuwa haijaguswa na moto hata kidogo na ndiyo maana ilikuwa gumzo kwenye vyombo vya habari.

“Ni muujiza! Miujiza haiachi kutokea,” alisema tajiri huyo mwenye umri wa miaka 64.

Related Posts