Dar es Salaam. Tanzania imeendelea kung’ara katika nyanja za kimataifa baada ya Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk John Rwegasha kuteuliwa kushika wadhifa wa Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Tiba, Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU).
Dk Rwegasha ambaye anatarajiwa kuanza kazi Februari 2025 katika nafasi hiyo mpya amesema anamshukuru Mungu kwa nafasi hiyo ambayo ilikuwa na ushindani mkubwa katika mchakato wa usaili.
Akiagana na Menejimenti ya MNH mwishoni mwa wiki hii, Dk Rwegasha amesema amefanikiwa kufaulu na kuteuliwa rasmi kati ya washindani wenzake kutoka mataifa saba ya Afrika.
Dk Rwegasha anatarajiwa kuanza kazi Februari 2025 kwenye Kamisheni hiyo ya AU yenye makao makuu Addis Ababa nchini Ethiopia.
Akitoa salamu za pongezi, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Mohamed Janabi ambaye pia ni mshauri wa Rais masuala ya afya na tiba amemtakia kila la kheri na uwakilishi mzuri wa Tanzania katika kutekeleza majukumu yake kwenye chombo kikubwa cha Umoja wa Afrika hususan eneo la afya barani Afrika.
Dk Rwegasha ni daktari bingwa mbobezi wa magonjwa ya mfumo wa chakula na ini ambaye kutokana na jitihada zake alifanikisha MNH kuanzisha kituo cha utoaji mafunzo na tiba ya ugonjwa huo nchini mwaka 2013.
Dk Rwegasha alikuwa Mkuu wa Kitengo hicho hadi mwaka 2018 alipoteuliwa kuwa mkuu wa idara ya magonjwa ya ndani yenye vitengo 11 na baadaye Oktoba 2022 aliteuliwa kuwa mkurugenzi wa huduma za tiba MNH, ambapo alikua akisimamia idara saba.
Kuhusu elimu Dk Rwegasha ana Shahada ya kwanza ya daktari ya Chuo Kikuu cha Makerere, Shahada ya Uzamili ya Udaktari ya Chuo Kikuu cha Aga Khan Kenya, Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Uongozi ya Chuo Kikuu Mzumbe.
Stashahada ya Usimamizi wa Afya ya Chuo Kikuu cha Washington, Marekani pamoja na utambulisho mwingine kadhaa wa kitaaluma katika tiba kutoka vyuo vikuu nchini Uingereza na Afrika Kusini.