MWENYEKITI wa Geita Gold, Leonard Bugomola amesema moja ya malengo waliyompa kocha mpya wa timu hiyo, Mohamed Muya ni kuhakikisha kikosi hicho kinacheza Ligi Kuu Bara msimu ujao, licha ya kutopata muda mrefu wa kukifundisha tangu mwanzo.
Muya amejiunga na Geita baada ya kutimuliwa Fountain Gate kufuatia kuchapwa mabao 5-0 na Yanga Desemba 29, mwaka jana, akienda kukifundisha kikosi hicho akichukua nafasi ya Amani Josiah aliyejiunga na maafande wa Tanzania Prisons.
Akizungumza na Mwanaspoti, Bugomola alisema wanaamini uwezo wa kocha huyo utaifikisha timu hiyo kufikia katika malengo yao waliyojiwekea ya kurejea tena Ligi Kuu Bara baada ya kushuka msimu uliopita, hivyo hawana wasiwasi wowote juu yake.
“Tulikuwa na mapendekezo mengi ya makocha mbalimbali waliotuma wasifu wao (CV), lakini Muya alituvutia na kupendezwa na kile tulichokubaliana, moja ya malengo yetu ni kuhakikisha tunashika moja ya nafasi mbili za juu zitakazoturejesha Ligi Kuu.”
Hadi anaondoka Geita Gold, Josiah aliiongoza timu hiyo katika michezo 14 ya Ligi ya Championship ambapo alishinda tisa, sare mitatu na kupoteza miwili, akiiacha nafasi ya pili na pointi 30, nyuma ya vinara Mtibwa Sugar yenye pointi zake 35.